MCAs wa UDA Nairobi wataka viongozi wao wawili waadhibiwe kwa kudai Sakaja alifadhili Azimio

MCAs wa UDA Nairobi wataka viongozi wao wawili waadhibiwe kwa kudai Sakaja alifadhili Azimio

NA WINNIE ONYANDO

MADIWANI wa Nairobi wa mrengo wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) wanataka chama hicho kiwachukulie hatua madiwani wawili kwa kudai kwamba Gavana Johnson Sakaja alifadhili mkutano wa kisiasa uliofanyika Kamukunji.

Madiwani hao wanataka kiongozi wa wachache katika bunge hilo la kaunti Anthony Kiragu na kiranja wa wachache bungeni Mark Mugambi wachukuliwe hatua kwa kudai kwamba gavana Sakaja alifadhili mkutano wa Azimio la Umoja-One Kenya uliofanyika wiki jana kwenye uwanja wa Kamukunji.

Wawili hao walidai kwamba Bw Sakaja alitoa pesa na kuidhinisha uwanja wa mkutano.

“Tunataka Bw Sakaja ajitokeze waziwazi na aseme ikiwa alifadhili mkutano wa kisiasa wa Azimio,” alisema Bw Kiragu akiwahutubia wanahabari siku chache zilizopita.

Madiwani hao wakiongozwa na Clement Kamaru (Kahawa Magharibi), Jeremiah Themendu (Kayole kati) na James Kariuki (Ruai) sasa wanataka wawili hao waadhibiwe.

“Tunataka wawili hao wajiuzulu kufuatia madai hayo. Huyu ni gavana wetu ambaye anafaa kuungwa mkono ndipo aweze kutimiza ahadi zake,” akasema Bw Themendu.

Wamesema kwamba waliwapa madiwani hao wawili siku mbili kuomba msamaha kufuatia madai hayo ila hawakutimiza.

“Hii ndio maana tukaamua kuchukua hatua kama hiyo,” akasema Bw Kariuki.

  • Tags

You can share this post!

Papa Francis aanza ziara yake rasmi Afrika

Spika Wetang’ula awataka wabunge wapitishe sheria ya...

T L