MCAs waenda TZ kufunzwa adabu

MCAs waenda TZ kufunzwa adabu

Na GEORGE MUNENE

MADIWANI 33 wa Kaunti ya Embu wamezua gumzo baada ya kuelekea Tanzania kwenda kujifunza namna ya kusema maneno matamu, yatakayowasaidia kushawishi wapigakura ili wahifadhi viti vyao 2022.

Madiwani hao pia wameenda nchi hiyo jirani kujifunza maadili mema. Ziara hiyo, hata hivyo, imezua ghadhabu miongoni mwa wakazi wa Embu, ambao wanasema ni uharibifu wa fedha za walipaushuru. Afisa wa Bunge la Kaunti ya Embu aliyeomba jina lake libanwe kutokana na hofu ya kusutwa na wawakilishi hao wa wadi, aliambia Taifa Leo kuwa kila diwani atapokea kitita kikubwa cha marupurupu kwa muda watakaokuwa mjini Arusha.

“Ni kweli madiwani tayari wameelekea Tanzania baada ya kuahirisha vikao vya bunge. Kila diwani atapokea Sh37,000 kila siku kwa ajili ya malazi na marupurupu mengineyo,” akasema afisa huyo.Madiwani hao pia wameandamana na Spika wa Bunge la Embu Josiah Thiriku, Karani wa Bunge Jim Kauma pamoja na maafisa kadhaa.

Madiwani hao watatumia zaidi ya Sh20 milioni katika ziara hiyo. Hiyo ni mara ya pili kwa madiwani hao kuelekea nchini Tanzania kwa ajili ya mafunzo ndani ya miezi mitatu mwaka huu.Wakazi wanasema kuwa madiwani hao wamekuwa wakisafiri nje ya nchi kwa lengo la kusaka hela za kampeni na kulipa mikopo wanayodaiwa.

“Madiwani hao wanafaa kushtakiwa kwa kutumia vibaya fedha za walipa ushuru,” akasema mwenyekiti wa chama cha wafanyabiashara tawi la Embu, John Mate.Bw Mate pia aliitaka Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuanzisha uchunguzi dhidi ya madiwani hao na kisha washtakiwe.Seneta wa Embu Njeru Ndwiga alishutumu madiwani hao kwa kuwa na mazoea ya kusafiri nje nchi mara kwa mara badala ya kuhudumia wakazi.

Madiwani hao pia wametumia mamilioni ya fedha kusafiri jijini Nairobi na Mombasa mwaka huu.Ziara hiyo inafuatia huku EACC ikinyemelea maafisa wa Bunge la Kaunti ya Bungoma kwa kufuja hela za walipa ushuru kupitia ziara hewa.

Karani wa Bunge la Kaunti ya Bungoma aliidhinisha malipo ya Sh510,000 kwa hoteli ya Javenture Limited ya jijini Kisumu mnamo 2018 kugharamikia ziara ya madiwani 25.Uchunguzi wa EACC ulibaini kuwa madiwani hao hawakwenda jijini Kisumu hivyo ziara hiyo ilikuwa hewa.

Hatima ya maafisa hao wa Bunge la Kaunti ya Bungoma sasa iko mikononi mwa Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (DPP) baada ya EACC kupendekeza wakamatwe na kushtakiwa.

You can share this post!

Zetech ndio mabingwa wapya wa karate katika mashindano...

Viongozi wasutwa kukosa kikao cha Jumuia ya Pwani

T L