Habari Mseto

MCAs wahimizwa kufuatilia matumizi ya fedha za kaunti

September 20th, 2020 1 min read

Na BRIAN OJAMAA

MABUNGE ya kaunti yametakiwa kuimarisha kamati za fedha ili zichunguze jinsi serikali za kaunti zinavyotumia pesa kikamilifu.

Spika wa Seneti, Bw Ken Lusaka alisema seneti imepigania pesa zaidi kwa kaunti na ni muhimu madiwani, kupitia kamati za fedha, kuhakikisha zinatumiwa vyema.

“Uwepo wa kamati zenye nguvu za fedha ndiyo njia ya pekee kuhakikisha serikali za kaunti zinatumia vyema pesa zinazopewa na serikali ya kitaifa,” alisema.

Akizungumza alipohudhuria mazishi Cheptais, eneobunge la Mt Elgon mnamo Ijumaa, Bw Lusaka alisema anafuraha seneti ilimaliza mzozo kuhusu mfumo wa kugawa pesa za kaunti na kwamba, ni jukumu la madiwani kuhakikisha pesa hizo zinatumiwa vyema.

“Ukosefu wa kamati zinazoweza kuchunguza matumizi ya pesa katika baadhi ya kaunti ndiyo sababu zinatumiwa vibaya na kuporwa,” alisema Bw Lusaka katika mazishi ya Joyce Boiyo.

Kamati ya maseneta 12 iliyosimamiwa na Seneta wa Bungoma Moses Wetangula na mwenzake wa Nairobi Johnson Sakaja ilihakikisha hakuna kaunti itapoteza pesa.

Bw Wetangula aliyehudhuria mazishi hayo aliafikiana na Bw Lusaka akisema seneti itaendelea kupigania kaunti.