Siasa

Mchakato wa BBI umewaletea Wakenya mahangaiko zaidi – Mudavadi

December 20th, 2020 1 min read

Na JUSTUS OCHIENG

KIONGOZI wa chama cha ANC, Musalia Mudavadi ameonya kuhusu uwezekano wa kukwama kwa shughuli za utoaji huduma katika afisi za umma ikiwa taifa halitakamilisha haraka mdahalo kuhusu mageuzi ya katiba kupitia mpango wa maridhiano (BBI).

Alisema mdahalo huo ambao umewateka Wakenya usiku na mchana unapaswa kukamilishwa haraka ili kutoa nafasi kwa serikali kushughulikia changamoto zinazokabili taifa.

“Mgomo wa wahudumu wa afya umechangia kukwama cha shughuli katika vituo vya afya vya umma kote nchini, ilhali serikali za kaunti zinakabiliwa na changomoto nyinginezo za kifedha baada ya hazina ya kitaifa kuchelewa kutoa Sh60 bilioni ambazo ni sehemu ya mgao wa Oktoba, Novemba na Desemba,” Bw Mudavadi akasema.

Alisema inasikitisha kuwa changamoto kama hizi zimewaathiri wananchi na zinapasa kushughulikiwa ilhali nguvu zote zinaonekana kuelekezwa kwa BBI kana kwamba ndio suluhu kwa matatizo yote yanayozonga taifa hili.

“Tunapaswa kuhakikisha watumishi wa umma wanafanya kazi kwa sababu mjadala kuhusu BBI umejivuta kwa muda mrefu. Watumishi wa umma wamejigawa kwa misingi ya wale wanaounga au kupinga BBI,” Mudavadi akasema.

Kiongozi huyo wa ANC alisema kwa miaka miwili sasa, Wakenya wametekwa akili na sarakasi ya BBI na kuwafanya kusahau masuala mengine muhimu yanayoathiri nchi.

“Tukamilishe mjadala huu kwa njia ya ustaarabu na kwa njia ambayo itawezesha maoni na mapendekezo ya pande zote kuhusu suala hili kusikizwa. Muhimu ni kwa Wakenya kusalia wakiwa wameungana ili kutoa mazingira faafu kwa ufufuzi wa uchumi ulioathirika na janga la Covid-19,” Bw Mudavadi akasema Jumamosi kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo.