Mchakato wa kumsaka mrithi wa Maraga kuanza Jumatatu

Mchakato wa kumsaka mrithi wa Maraga kuanza Jumatatu

Na RICHARD MUNGUTI

MCHAKATO wa kumsaka Jaji Mkuu wa tatu tangu Katiba mpya ya 2010 izinduliwe utaanza rasmi Jumatatu hii.

Atakayefaulu kumrithi Jaji Mkuu (mstaafu) David Maraga atakuwa na kibarua kigumu ikiwa ni pamoja na kuamua kesi ya uchaguzi wa urais wa 2022 iwapo itawasilishwa.

Katika taarifa iliyotolewa na Tume ya Kuajiri Watumishi wa Idara ya Mahakama (JSC), harakati za kumsaka mrithi wa Bw Maraga zitaanza kwa kupokea maombi ya wale wanaohitimu kwa mujibu wa Kifungu nambari 166 cha Katiba.

Kiti cha Jaji Mkuu kiliachwa wazi kufuatia kustaafu kwa Bw Maraga mnamo Januari 12 2021.

Mnamo Januari 11 2021 Bw Maraga alimkabidhi Naibu wake Jaji Philomena Mwilu mamlaka ya kuwa kaimu Jaji Mkuu katika hafla iliyotangulia kustaafu kwake katika Mahakama ya Juu Nairobi.

Kulingana na sehemu ya 5 ya sheria za idara ya mahakama naibu wa Jaji Mkuu atahudumu kama Jaji Mkuu hadi mwingine ateuliwe.

Jaji Mwilu atahudumu katika wadhifa kwa muda wa siku 120 kabla ya JSC kumteua atakayemrithi Bw Maraga.

“Tunawahakikishia wananchi kwamba mchakato wa kumteua Jaji Mkuu mpya utakuwa na uwazi.Utaendelezwa kwa misingi ya sheria,” JSC ilisema katika taarifa iliyotoa Januari 15, 2021 kwa wanahabari.

JSC ilisema itakitangaza wazi kiti cha Jaji Mkuu wazi mnamo Januari 18,2021 kisha “ ianze kupokea maombi ya wanaotaka kuwania wadhifa huo.”

Baada ya kupokea maombi wote watakaoteuliwa majina yao yatachapishwa katika magazeti huku kila mmoja wao akitengewa siku ya kufika mbele ya wanachama wa JSC kuhojiwa.

Baada ya kukamilisha mahojiano wanachama watajitenga faraghani kumteua mshindi. Jina la atakayeteuliwa litapelekwa kwa Rais Uhuru Kenyatta kuapishwa.

Kiti cha Jaji Mkuu kitawafutia wawaniaji wa Mahakama ya Juu , Mahakama ya Rufaa, Mahakama kuu na pia mawakili walio na tajriba ya juu.

Jaji Mwilu, 62 atakuwa huru kuwania wadhifa huo wa Jaji Mkuu. Kuna msukumo wa mawakili wenye tajriba ya juu Jaji Mwilu ateuliwe moja kwa moja kuwa Jaji Mkuu.

Hata hivyo Majaji wa Mahakama ya Juu watakaowania wadhifa huo ni, Jaji Smokin Wanjala, Jaji Njoki Ndung’u na Jaji Isaac Lenola.

Wengine wanaotazamiwa kuwasilisha maombi yao ni rais wa mahakama ya rufaa Jaji William Ouko. Pia Jaji Mbogholi Msagha wa Mahakama kuu.

Wengine wanaomezea mate kiti cha hicho ni mwanasheria mkuu Jaji (mstaafu) Paul Kihara Kariuki, Prof Githu Muigai, mawakili Philip Murgor, Ahmednassir Abdullahi na Abdi Kadir.

Wengine wanaotazamiwa kuomba wadhifa huo ni pamoja na wakili mwenye tajriba ya juu anayeishi Amerika Profesa Makau Mutua.

Wanachama wa JSC sasa ni Philomena Mwilu, Jaji Mohamed Warsame, Jaji David Majanja, Jaji (mstaafu) Paul Kihara Kariuki,Evalyne Olwande (hakimu anayewakilisha mahakimu) , Dkt Mercy Mwara Deche, Macharia Njeru (mwakilishi wa chama cha wanasheria nchini), Felix Kiptarus, Prof Olive Mugenda na msajili wa mahakama Anne Amadi.

Atakayeteuliwa kuwa Jaji Mkuu lazima awe amehudumu kwa miaka 15 kama Jaji wa aidha mahakama ya rufaa au mahakama kuu.

Endapo ni wakili atakayeteuliwa lazima awe amehudumu kama rais wa chama cha wanasheria nchini na pia awe anaweza kuteuliwa moja kwa moja kuwa jaji wa mahakama ya rufaa.

You can share this post!

Zifahamu faida za hiliki

EU yasifu uchaguzi wa Uganda