Habari

Mchakato wa kura ya maamuzi 'kuiva'

July 19th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

UAMUZI kuhusu iwapo kura ya maamuzi ya ‘Punguza Mzigo’ itafanyika au la utatolewa mwishoni mwa Juni 2020.

Hii ni kulingama na utaratibu uliowekwa na Katiba ya sasa kuhusu namna ya kufanikisha marekebisho ya Katiba yanayoathiri kipindi cha kuhusu kwa Rais na muundo wa bunge, kama inavyopendekezwa chini ya mpango huu unaodhaminiwa na chama cha Thirdways Alliance.

Mswada wake ulioidhinishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Alhamisi, sasa utawasilishwa kwa Maspika wa Mabunge 47 ya kaunti kuushughulikia ndani ya siku 30.

Kulingana na kipengee cha 257 (5), mswada huo wa mchakato wa ‘Punguza Mzigo’ utawasilishwa, kwa pamoja, katika bunge la Kitaifa na Seneti ikiwa utapitishwa na angalau mabunge 24 ya kaunti.

Endapo IEBC iliwasilishwa mswada huo kwa Maspika wa mabunge yote ya kaunti Ijumaa, ina maana kwamba mabunge hayo yana muda wa hadi Oktoba 18 kuupitisha au kuukataa.

Katika mabunge hayo mawili, mswada huo utashughulikiwa kwa kipindi cha siku 90, sawa na miswada ya kawaida.

Hii ina maana kuwa uamuzi wa Bunge la Kitaifa na Seneti kuhusu mswada huo, unaodhaminiwa na chama cha Thirdways Alliance, utatolewa mwishoni mwa mwezi Machi 2020.

Na, endapo mswada huo utapitishwa na mabunge hayo kwa kura ya wengi, Rais Uhuru Kenyatta atautia saini na kuamuru uchapishwe kuwa sheria.

Kwa hivyo, hapata kuwa na haja na kuandaliwa kwa kura ya maamuzi ambayo inakadiriwa kuigharimui serikali angalau Sh15 bilioni.

Kura ya maamuzi

Lakini endapo utakataliwa ama na Bunge la Kitaifa au Seneti, mswada huo utawasilishwa kwa umma kuwa kura ya maamuzi ambayo itaendeshwa na IEBC.

Kulingana na kipengee cha 256 (5) cha Katiba tume hiyo itahitajika kuandaa kura hiyo ndani ya kipindi cha siku 90.

Ikiwa hilo litafanyika, ina maana kuwa shughuli hiyo itafanyika mwishoni mwa Juni 2020 baada ya kusomwa kwa Bajeti ya Kitaifa ya mwaka ujao wa kifedha wa 2020/2021.

Kulingana na kipengee cha 255, ibara ya (5) (a) na (b) mswada wa marekebisho ya katiba kwa njia ya kura ya maamuzi sharti upate uungwaji mkono kutoka angalau asilimia 20 ya wapiga kura katika kaunti 24 au zaidi.

Mswada huu pia unaweza kuwa sheria ikiwa utapigiwa kuwa na wengi wa wapiga kura watakaoshiriki kura ya maamuzi anavyosema wakili wa sheria ya kikatiba Bobby Mkangi.

“Hii ni kwa sababu mswada huu wa ‘Punguza Mzigo’ unalenga kupunguza kipindi cha kuhudu kwa Rais na muundo wa bunge kama asasi,” Bw Mkangi ameambia Taifa Leo Ijumaa kwenye mahojiano ya simu.

Baada ya mswada huo kupitishwa katika kura ya maamuzi Mwenyekiti wa IEBC Bw Wafula Chebukati atauwasilisha kwa Rais Kenyatta, ndani ya siku 30 baada ya kukamilika kwa zoezi hilo.

Utachapishwa kuwa sheria baada ya kupata sahihi ya Rais.

Hata hivyo, wadadisi wanasema kuwa mswada huo unatarajiwa kupata upinzani mkubwa katika bunge la kitaifa, hasa miongoni mwa wabunge wa kike.

Hii ni kwa sababu unapendekeza kufutuliwa mbali kwa nyadhifa Wabunge Wawakilishi wa Wanawake 47.

Vilevile, mchakato huo wa ‘Punguza Mzigo’ unataka kuondolewa kwa nafasi za wabunge na madiwani maalum, wengi wa wakiwa wanawake.

“Upinzani huo utatiwa moto na makundi wa wanaharakati wa kutetea haki wa wanawake kama vile Chama cha Mawakili Wanawake (Fida) na Maendeleo ya wanawake,” anasema Bw Javas Bigambo ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa.

“Isitoshe, baada ya wabunge wanaume watapinga mswada huu kwa sababu utachangia wao kupoteza nafasi ya kurejea bungeni. Lakini hawatafaulu kwa sababu seneti imeuunga mkono kutokana na pendekezo ya kuipa mamlaka makuu,” anaongeza.

Wakili Mkangi anaongeza kuwa huenda watu fulani watajaribu kuvuruga mpango huu kwa kuwasilisha kesi kortini kupinga uhalali wa IEBC.

“Watu fulani tayari wameanza kunong’oneza kuwa tume hii makamishna watatu hawana idhini kisheria kufanya maamuzi makubwa kiasi cha kuitisha kura ya maamuzi. Hii ni kwa sababu kisheria uamuzi kama huu unapasa kupitishwa na angalau makamishna watano,” anasema.