Mchanga wa ufuoni unavyotia ladha njugu

Mchanga wa ufuoni unavyotia ladha njugu

KWA kawaida, mchanga mweupe wa baharini katika Pwani za Kenya huaminika kuwa sehemu ya kivutio kikuu cha utalii.

Lakini kwa wakaangaji na wauzaji njugu, mchanga huo ni kiungo muhimu cha mapishi yao.

Mabw Charles Kiama na Dennis Maundu kutoka eneo la Changamwe, Kaunti ya Mombasa, ni baadhi ya wakaanga njugu wanaotumia mchanga huo kuzipa njugu zao ladha ya kipekee.

Wawili hao ambao wamekuwa wakifanya biashara hiyo kwa takriban miaka miwili sasa, wanaeleza kuwa, mchanga huo husaidia pia kuhakikisha kuwa njugu zao haziungui.

“Mchanga wa bahari tunaotumia husaidia sana kuhakikisha kuwa zinapata joto kwa usawa na basi haziungui. Pia huzipa ladha ya kipekee,” anasema Bw Kiama.

Kwa kawaida, njia ya kukaanga njugu inayojulikana huwa ile ya kutumia sufuria au karai pekee inayoekwa juu ya jiko la moto.

Kulingana na mchuuzi ambaye hununua njugu hizo ili aende kuziuza kwa rejareja, Bi Bahati Odongo, njugu zinazopikwa kwa mbinu hiyo huvutia wateja wengi.

Hata hivyo, aliungama kwamba ni mbinu ngumu, ghali na mara nyingine kwa wasioifahamu kuitumia, huharibu ladha.

“Nimekuwa mteja wa vijana hawa kwa kuwa wanaponiuzia nina hakika wateja wangu watafurahia. Njugu haziungui wala kuharibika ikilinganishwa na iwapo ningekaanga nyumbani,” akasema Bi Odongo.

Kwa mujibu wa sayansi, mchanga wa baharini huwa una uwezo wa kupokea joto kwa usawa. Njugu ambazo huwa juu ya mchanga hupokea joto na kuiva bila kuungua.

“Tunapoweka mchanga ambao ni safi tunakaanga njugu kwa muda kiasi na tukiona umebadilika rangi tunajua umeshachafuka na ni vyema kuubadilisha,” anasema Bw Maundu.

Walieleza kuwa, mchanga huo hutolewa katika sehemu za kipekee baharini ili kuhakikisha siyo sawa na ule wanaokanyaga watu ufuoni.

Magwiji hao wa kukaanga njugu wanaeleza walianza biashara hiyo, baada ya kumfanyia kazi mfanyabiashara mwingine.

Charles Kiema, Mkaanga Njugu kutoka eneo la Changamwe akiendelea na shughuli zake za kila siku katika picha hii iliyopigwa Machi 15, 2023. PICHA | KEVIN ODIT

Licha ya wachuuzi wengi kununua kwao kabla ya kuzifunga kwa mifuko midogo, wanaeleza kuwa gharama ya maisha imeathiri biashara hiyo.

Hapo mwanzoni walikuwa wakikaanga takriban magunia manne ya njugu, ila sasa hata kufikisha nusu ni ngumu kwa vile bei ya njugu mbichi imepanda.

“Tukipandisha bei hata sisi, wanunuzi wadogo wanalia na kupunguza ununuzi wao,” anasema Bw Kiama.

Taifa Leo ilibaini kuwa mtindo huo wa ukaangaji unatumiwa katika sehemu kadha za Kaunti ya Mombasa.

Biashara hunoga zaidi kutokana na jinsi watafunaji wengi wa muguka huchanganya majani yao na njugu.

  • Tags

You can share this post!

Kisanga kituo cha polisi Nakuru wanaume 2 wakihubiri juu ya...

Wabunge wa Kenya Kwanza wadai maandamano ya Raila ni sawa...

T L