Mchecheto mitandaoni Karen Nyamu akijaribu kumnasa Samidoh

Mchecheto mitandaoni Karen Nyamu akijaribu kumnasa Samidoh

Na SAMMY WAWERU

Mwanamuziki tajika wa nyimbo za Benga kwa lugha ya Agikuyu, Samuel Muchoki maarufu kama Samidoh amejipata kwenye njia panda na mashibiki wake wanaomfuatilia kwenye mitandao ya kijamii.

Hii ni baada ya mwanasiasa mmoja wa jiji la Nairobi, Karen Nyamu, Jumamosi kuthibitisha kuwa Samidoh ndiye baba ya mwanawe wa pili.

Kwenye kurasa zake za mitandao, Nyamu ambaye katika uchaguzi mkuu wa 2017 aliwania kiti cha mwakilishi wa wanawake Nairobi, alipakia video fupi ya mwimbaji huyo akiwa amepakata mwanawe ambaye ni mvulana.

“Baba hakuelezi kwamba anakupenda, anathibitisha kwa matendo #Muchokis,” maandiko ya Karen yakaandamana na chapisho hilo.

Hatua ya wakili huyo, hatimaye iliondoa shauku ya muda wa miezi kadhaa kuhusu nani ndiye baba ya mwanawe huyo wa pili.

Mwaka uliopita, 2020, akiwa mjamzito, Karen alikuwa akipakia kwenye kurasa zake za mitandao picha za wawili hao wakiwa pamoja.

Samidoh na ambaye ni afisa wa polisi ana mke na watoto wawili.

Mitandaoni, ikifichuka mkewe ambaye wapekuzi wamemtambua kama Edday Nderitu na Karen wanaendelea ‘kuvuana nguo’ kwa kurushiana maneno mazito hadharani.

Baada ya kujifungua, Karen alinukuliwa akisema “nitakuwa nikipakia video na picha za baba ya mwanangu wakati ninaotaka”.

Aidha, Karen ameweka paruwanja hatakoma kuchapisha picha za familia yake mitandaoni, na kwamba hana chochote cha kuficha kuhusu familia yake.

Ni matukio ambayo yamezua mdahalo mkali mitandaoni, wengi wa mashabiki wa Samidoh wakimkashifu na kumshika koo.

“Huyu Samidoh akiendelea kucheza, karia yake katika muziki itaanguka,” #Mary George akasema.

“Machozi yanamsubiri,” Gracie Macharia akaelezea, akizua utani.

Cyrus Prop Koech akapendekeza: “Samidoh anapaswa kufanya maisha yake binafsi yawe ya faragha. Aige mfano wa Nameless na Wahu.”

Huku wengi wa waliotoa maoni wakiwa wanawake, wakieleza ghadhabu zao kwa kile walihoji Samidoh amesaliti mke wake, Estah Shiroh alisema ni aibu kwa staa huyo kuhalalisha hadharani uhusiano haramu kati yake na Karen.

“Hata haogopi anavyohisi mke wake. Ikiwa angemdhibiti mpango wake wa kando, asingekuwa na ujasiri kuhutubia ulimwengu,” #Estah Shiroh akasema.

Jane Nyawira akaongeza: “Ni muhimu watu kuishi maisha ya siri (akimaanisha kuficha masuala ya familia na uhusiano), ili kuepuka kukwaza mwenzako. Wakati mwingine hekima haijiri na umri, ila tajiriba.”

Licha ya wengi kukashifu Samidoh, kuna kadha waliounga mkono uhusiano wake na Karen. “Wanawake, tulisema tunagawana kwa amani. Wanaosema ataishia kwa kilio na majonzi, waangalie muktadha wa uhusiano wao kwa njia tofauti,” Lucy Wanjiru akachangia.

“Umewadia wakati wanawake waitikie ndoa za zaidi ya mke mmoja, kama walivyofanya kina babu na nyanya zetu. Bora mume anakimu mahitaji ya wake na wanawe, sioni hatia iliyoko,” Lastriq Njau akaelezea, akionekana kutetea hatua ya msanii huyo.

Awali, Samidoh alikuwa amekana kuhusu uhusiano wake na Karen, ila sasa mtama umemwagwa kwa kuku, ambao ni wengi na unavyoelewa ni nadra kushiba hadi nafaka itakapoisha. Nafaka ikiisha wataashiria kutaka nyongeza.

Samidoh anafahamika kwa nyimbo zinazoongoa mashabiki wake katika jamii ya Kikuyu kama vile Ndiri Mutwe (sina kichwa/akili timamu), Kairitu Gakwa (binti yangu), Wendo Wi Cama (upendo wenye raha na tamu), kati ya vibao vinginevyo.

You can share this post!

Kampuni za humu nchini haziruhusiwi kuagiza chanjo –...

Soko ya Daraja la Pili yapamba moto Pwani