Mchecheto PSG jeraha likitishia kumweka nje Mbappe katika marudiano dhidi ya Man-City kwenye UEFA

Mchecheto PSG jeraha likitishia kumweka nje Mbappe katika marudiano dhidi ya Man-City kwenye UEFA

Na MASHIRIKA

PARIS Saint-Germain (PSG) wana mchecheto mkubwa kadri wanavyosubiri kufahamu hali ya fowadi Kylian Mbappe anayetazamiwa kuwa katika fomu ya kumwezesha kupangwa katika kikosi kitakachorudiana na Manchester City katika nusu-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) usiku wa leo ugani Etihad, Uingereza.

Mshambuliaji huyo raia wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 22, alikosa mechi ya wikendi iliyopita iliyowakutanisha PSG na Lens katika kipute cha Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1).

Kocha Mauricio Pochettino amekiri kwamba hali ya Mbappe ambaye ni mfungaji wa PSG msimu huu, itatathminiwa na madaktari kabla ya maamuzi ya mwisho kuhusu iwapo atachezeshwa dhidi ya Man-City kufanywa.

“Ataangaliwa tena na madaktari pindi tutakapowasili jijini Manchester. Alirejelea mazoezi mepesi mnamo Jumamosi na tuna matarajio kwamba atakuwa amepona kabisa,” akasema Pochettino.

Mbappe amefungia PSG jumla ya mabao 37 kutokana na mechi 43 zilizopita katika mapambano yote ya msimu huu, yakiwemo magoli 10 kwenye kivumbi cha UEFA.

PSG watatua Etihad wakiwa na kibarua kigumu cha kubatilisha kichapo cha 2-1 walichopokezwa na Man-City katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa nusu-fainali ya UEFA uwanjani Parc des Princes, Ufaransa wiki moja iliyopita.

Miamba hao wa Ligue 1 wanapania kutinga fainali ya UEFA kwa msimu wa pili mfululizo baada ya kuzidiwa maarifa na Bayern Munich waliowapiga 1-0 kwenye fainali ya msimu wa 2019-20 jijini Lisbon, Ureno.

Sawa na PSG waliowapepeta Lens 2-1 katika mchuano wao uliopita kwenye Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1), Man-City pia watajibwaga ugani wakijivunia motisha ya kusajili ushindi wa 2-0 dhidi ya Crystal Palace katika pambano lao lililopita la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ugani Selhurst Park.

Baada ya kubanduliwa kwenye hatua ya robo-fainali za UEFA kwa misimu mitatu iliyopita mfululizo, Man-City wanatarajiwa kujituma zaidi mara hii na kuingia fainali itakayowakutanisha ama na Chelsea au Real Madrid mnamo Mei 29 uwanjani Ataturk Olympic, Uturuki.

Man-City hawana visa vyovyote vya majeraha huku Guardiola akiwapumzisha masogora Ilkay Gundogan, Kevin de Bruyne, Riyad Mahrez, Bernardo Silva, Kyle Walker, Ruben Dias na Phil Foden katika mechi iliyopita ya EPL dhidi ya Crystal Palace ugani Selhurst Park

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

SHINA LA UHAI: Mto Ewaso Ng’iro hatarini kukauka

Mbona tusiwajaribu?