Bambika

Mchekeshaji Dkt Cassypool adai ni chawa wa Rais

March 6th, 2024 2 min read

NA JURGEN NAMBEKA

MCHEKESHAJI mwenye sifa na ufuasi mkubwa mtandaoni, Dkt Cassypool, amewarai vijana kutoka ukanda wa Pwani na Kenya kwa ujumla kuchangamka na kutumia fursa zilizoko katika sekta mbalimbali kujiendeleza maishani.

Dkt Cassypool ambaye jina lake halisi ni Kevin Odhiambo Onyango, alisema vijana wanafaa kujituma na kujitajirisha kupitia sekta ambazo awali zilidhaniwa kuwa za wazee tu.

Akizungumza baada ya kuzinduliwa kwa tawi jipya la kampuni ya uchukuzi na usafirishaji wa mizigo ya Nemis ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikifanyia shughuli zake nyingi nchini Tanzania, alieleza kuwa vijana wanapaswa kupevuka macho na kujiamini ili kufanya mambo makubwa kwa kuwa serikali ya Kenya Kwanza chini ya Rais William Ruto imeonyesha kwamba iko tayari kuwaunga mkono.

“Jinsi mnavyofahamu, mimi ni chawa wa rais na leo nimefika hapa Mombasa kwa uzinduzi wa kampuni hii ambayo inalenga kufungua njia kwa ajili ya vijana. Mkitazama hapa hata Afisa Mkuu Mtendaji pamoja na washirika wenzake, ni vijana. Hii ni ishara tosha kuwa hata vijana wadogo sana wanaweza kufanikisha malengo yao wakiwa na lengo thabiti,” akasema Dkt Cassypool.

Mchekeshai huyo ambaye sasa ametia saini mkataba na kampuni hiyo kama balozi wa kuitangaza na kuieneza nchini, alieleza kuwa sasa kampuni hiyo itawalenga sana vijana, ambao wengi hawajafanikiwa kupata nafasi za ajira.

Mchekeshaji Dkt Cassypool (kati) ambaye jina lake halisi ni Kevin Odhiambo Onyango akihutubia wanahabari akiwa jijini Mombasa baada ya kuzinduliwa kwa tawi jipya la kampuni ya uchukuzi na usafirishaji wa mizigo ya Nemis ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikifanyia shughuli zake nyingi nchini Tanzania. PICHA | JURGEN NAMBEKA

Naye Afisa Mkuu mtendaji wa Nemis Edward Mwela alieleza kuwa licha ya kampuni kadhaa kutoka mataifa mengine kuwa na wasiwasi na kuondoka nchini, alikuwa na imani ya kupiga hatua kwani wateja wa kampuni hiyo nchini Tanzania walioamua kutumia bandari ya Mombasa wanahitaji usaidizi wa kushughulikia na kusafirisha mizigo yao.

“Wanabiashara wengi wamehamia nchini Kenya kwa sababu ya kazi nzuri inayofanywa na Mamlaka ya Kusimamaia Bandari Nchini (KPA) hasa katika Bandari ya Mombasa. Inachukua muda mchache kupakua mizigo kutoka kwa meli. Ndiposa tumetua huku na kufungua afisi hii hapa Mombasa na nyingine tunayolenga kufungua katika jiji kuu Nairobi ili kuhakikisha kuwa tunawashughulikia wateja wetu na pia Wakenya ambao watapata nafasi za ajira,” akasema Bw Mwela.

Mkuu huyo alisema kampuni hiyo iko tayari kuwapa fursa vijana ambao hawana ujuzi mwingi katika kazi hiyo, ili wapate sehemu ya kuanzia ikikumbukwa kuwa sekta nyingi huwataka wafanyakazi wenye ujuzi wa miaka mingi ya kutekeleza biashara husika.

“Tumewachagua vijana ili tuweze kukua nao. Wapate ujuzi na maarifa wakiwa nasi. Tutakuwa pia tukitoa vibarua mara kwa mara na hata pia kuwapa vijana wanaotuletea biashara ya usafirishaji komisheni ili wajiendeleze,” akasema Bw Mwela.

Mkurugenzi wa Nemis Jennifer Wairimu alieleza kuwa kampuni hiyo imekuwa ikitekeleza kazi hiyo ya kupokea na kusafirisha mizigo kwa miaka kadhaa ila humu nchini ina miezi miwili kati ya usajili na uzinduzi wake.

“Kwa sasa tuko tayari kwa biashara na kwa kuwa kampuni hii inaelekezwa na vijana, tunajua wateja zaidi watatuamini na kutupa kazi. Hii ni katika hali ya vijana kuweka juhudi ili tujitafutie tonge katika zile sekta ambazo awali hatukuwa tumeingia,” akasema Bi Wairimu.

Kwa mujibu wa wakuu na wasimamizi wa kampuni hiyo kutoka humu nchini na taifa jirani la Tanzania, kampuni hiyo iko tayari kuhakikisha kuwa mtazamo wa vijana unabadilika kwa kuanzisha mikakati baina yao ambayo inaweza ikaleta mabadiliko na fursa za wao kujiendeleza.