Bambika

Mcheshi Butita atishia kuuza gari kwa kusengenywa eti amewekwa na ‘mumama’

April 4th, 2024 1 min read

Na SINDA MATIKO

Butita awaza kuliuza gari lake la 5M Jaguar XE kisa madai ya ‘limama’

TOKA penzi lake na mchekeshaji mwenza Mamitto lilipoingia nyongo na kuvunjika baada ya takriban miaka saba, mvunja mbavu Eddie Butita kahusishwa na wanawake kibao.

Butita amekuwa akihusishwa kuwa kwenye mapenzi na influensa Sadia Said ingawaje wawili hao licha ya kuonekana kwenye mitoko kadhaa pamoja, hawajawahi kuweka wazi aina ya mahusiano yao.

Aidha pia kumekuwa na tetesi kuwa toka Butita atemane na Mamitto, amekuwa akiwekwa na ‘limama’ lenye mkwanja na ndio sababu maisha yake yanaonekana kubadilika pakubwa siku za hivi karibuni.

Hii ikiwa madai ya kununuliwa ndinga yake ya nguvu aina ya Jaguar XE yenye thamani ya Sh5 milioni.

Kabla ya kumilikia Jaguar XE, Butita alikuwa alimilikia gari la kiwango cha chini kidogo Nissan Tilda lenye thamani ya Sh850,000 ambalo ndilo alikuwa akionekana nalo mara kwa mara likimrahisishia kupiga misele mjini.

Jitihada za kujitetea kwamba aliinunua Jaguar XE kwa fedha zake, bado hazijaonekana kufua dafu na sasa Butita anasema anawaza kuliuza gari hilo na kisha kununua lingine la bei mbaya zaidi ili kuwakomoa wanoko wanaomsema kivingine.

“Nafikiri itafika muda nilazimike kuliuza gari hili maana nimechoka na hizi taarifa za kubuni. Hivi ni kwa nini watu hawana imani na kazi zetu hizi? Jamani nimefanya vitu vingi tu, tena miradi mikubwa zilizoniingiza fedha za kutosha. Kuna hata kipindi Rais mwenyewe alisema ninatengeneza mkwanja kuliko mshahara wake kabla ya makato ya kodi,” Butita kateta.

Staa huyo aidha kaendeleza masikitiko yake kwa namna watu wanavyoonekana kumdharau.

“Kwani mimi siwezi kujituma nikapata fedha za kutosha za kuniwezesha kumiliki gari zuri. Lazima iwe eti nimemilikishwa na limama. Jamani mambo mengine kama haya hayanikai kichwani,” ameongeza.

Kulingana na Butita, chanzo cha taarifa hizo ni mitandao ya kijamii anakosema kuna watu waliamua kuunga unga habari za uwongo punde alipotangaza kuwa amechomoa mchuma mpya.