Habari Mseto

Mcheshi Kiengei na mbunge wa zamani ‘washikana mashati’

April 14th, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

MWANZILISHI wa kanisa la Jesus Compassion Ministries (JCM), Pasta Benson Kiengei, wikendi alizua gumzo katika mitandao ya kijamii, baada ya mzozo mkali kuibuka baina yake na aliyekuwa mbunge wa Gatundu Kaskazini, Bi Wanjiku Kibe.

Mzozo huo ulianza baada ya Pasta Kiengei kudai kwamba Bi Kibe alimfuta kazi alipokuwa mkuu wa kituo kimoja cha redio alichokuwa akifanyia kazi (alikorejea na anahudumu hadi sasa).

Bw Kiengei alimlaumu mwanasiasa huyo kwa “kuendelea kumdharau hata baada ya Mungu kumbariki, baada ya kufungua kanisa lake na kupata ufuasi mkubwa.

“Bi Wanjiku Kibe, naamua kukuheshimu, licha ya yale uliyonifanyia 2012 nilipojiunga na kituo cha redio cha Kameme. Wakati huo, ndiwe ulikuwa mkuu wa kituo hicho. Hata hivyo, hatua yako kuligusa kanisa la JCM kwa sababu washindani wako wa kisiasa huwa wanatutembelea imenifanya kuelekeza machungu yangu kwako,” akasema Bw Kiengei, ambaye pia ni mcheshi, kwenye ujumbe alioandika katika mitandao ya kijamii.

Kwenye ujumbe wa hapo awali, Bi Kibe aliweka video ambapo mcheshi huyo alidai kwamba ndiye alimsaidia mbunge wa sasa wa Gatundu Kaskazini, Bw Elijah Kururia, kuibuka mshindi.

“Kumbe [Kiengei] ndiye alitusaidia kupata mbunge 2022. Sikuwa najua,” akasema Bi Kibe kwenye ujumbe uliojaa kejeli.

Mchesh Kiengei, kwa upande wake, alidai kuwa mwanasiasa huyo ndiye alichangia afutwe kazi kwa madai ya “kuwa mchafu na kutojua kazi ya utangazaji”.

“Ulichangia na kuchochea kufutwa kwangu. Njoo hapa na ueleze ikiwa ninaeleza uwongo,” akasema.

Hata hivyo, Bi Kibe alimtaka mcheshi huyo kueleza ukweli, akisema kuwa alijaribu kumtetea, kwani ndiye “aliyetambua kipaji chake cha ucheshi kwenye mashindano yaliyokuwa yakiendeshwa na kituo hicho”.

“Ni wakati tujifunze kuongea ukweli. Ni vipi ningechangia kufutwa kwa mtu ambaye mimi binafsi nilimtambua kuwa na kipawa cha ucheshi. Nakuomba kuwaeleza mashabiki wako ukweli,” akasema Bi Kibe.

Kutokana na majibizano baina ya watu hao wawili wenye ufuasi mkubwa katka mitandao ya kijamii, mashabiki wao pia waligawanyika, huku wakielekezeana matamshi makali makali.