Bambika

Mcheshi Muthee Kiengei sasa kutawazwa kuwa Askofu

March 6th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

NI dhahiri sasa kuwa Pasta Ben Gathungu almaarufu ‘Muthee Kiengei’ atatawazwa kuwa Askofu.

Kulingana na tangazo lililotolewa na kanisa lake la Jesus Christ Compassion Ministries (JCM) mnamo Jumanne, mcheshi huyo atatawazwa kuwa Askofu Juni 21, 2024.

Mcheshi huyo, anatawazwa kuwa askofu mwaka mmoja na miezi kadhaa baada ya kulifungua Kanisa hilo mwaka 2023.

“Ni rasmi sasa. Askofu Mteule wa Kanisa la JCM. Tunaanza kuhesabu siku leo. Mungu huwa anaufanya msimu wake kuwa wa kuvutia,” akasema mcheshi huyo, kwenye ujumbe alioweka katika kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Hatua ya mcheshi huyo kuanzisha Kanisa lake imeonekana kuwachochea ‘macelebs’ wengine maarufu katika ukanda wa Mlima Kenya kuanzisa makanisa yao.

Miongoni mwao ni mwanamuziki Sammy Irungu, ambaye majuzi alianzisha Kanisa lake la Mountain of Refuge Christian Centre (MRCC) na Askofu Paul Kuria miongoni mwa wengine wengi.

Muthee Kiengei ameshikilia kuwa nia ya kuanzisha Kanisa lake ni kuendeleza “injili ya kuwasaidia watu wasiojiweza katika jamii”.

Amekuwa akishikilia nia ya Kanisa lake ni kuchukua mkondo tofauti, kwa kuhakikisha kwamba washirika wake wanafaidika, badala ya mtindo wa sasa, ambapo asilimia kubwa ya pesa ambazo hutolewa makanisani huchukuliwa na wengi kuwa zinatumika kuwanufaisha wahubiri.

“Nia yetu ni kubadilisha uenezaji injili nchini. Hili ni kwa kuhakikisha kuwa kando na kuwafaidi washirika wetu kiroho, tunawafaidi pia kimahitaji,” akasema.

Kufikia sasa, Kanisa hilo lina matawi kadhaa katika maeneo kama Nyahururu, Nyeri, Nakuru, Embu, Narok kati ya sehemu nyinginezo.

Mcheshi huyo alianzisha kanisa lake baada ya kufurushwa kutoka kanisa jingine alikokuwa akihudumu kama kasisi.