Habari Mseto

Mchina aliyetusi Uhuru na kuita Wakenya 'nyani' aona cha moto

September 6th, 2018 2 min read

PETER MBURU na WINNIE ATIENO

SERIKALI Alhamisi ilimkamata na kumsafirisha raia wa China ambaye alirekodiwa kwa video akiwatusi Wakenya na kumwita Rais Uhuru Kenyatta ‘nyani’.

Kwenye video iliyosambaa mitandaoni na kuibua hasira miongoni mwa Wakenya, Bw Liu Jiaqi anawatusi wananchi kuwa masikini na wajinga, huku akimzomea mfanyakazi.

“Wakenya wote ni kama nyani, mnaweza kwenda kortini mnifunge,” akasema.

Raia huyo aidha alitumia maneno mengine mengi ya matusi hata kwa Rais Kenyatta, na kudunisha Kenya akisema amekuja huku tu kutafuta pesa.

“Hati zake za kufanya kazi humu nchini zimefutiliwa na atarejeshwa kwao hii leo kwa kuendeleza dhuluma za rangi. Idara ya uhamiaji aidha itasafirisha Wachina wengine 13 ambao walikamatwa katika kituo cha studio za runinga ya CGTN ambao wamekuwa nchini kwa njia haramu,” ikasema habari kutoka kwa msemaji wa serikali Erick Kiraithe.

Kitendo cha Mchina huyo awali kilikuwa kimeibua ghadhabu tele miongoni mwa Wakenya wakitaka akamatwe na kupelekwa seli, kabla ya kutimuliwa nchini, huku wengi wakilaumu ufisadi kuwa umefanya watu wasio na maadili kuruhusiwa kuingia nchini kudunisha wananchi.

Kwingineko, maafisa wa upelelezi eneo la Pwani walianzisha msako dhidi ya raia wa kigeni wanaoishi na kufanya kazi kinyume na sheria na wale wasiokuwa na vibali.

Aidha msako huo unalenga wale wanaofanya kazi katika sekta ya utalii, magari na viwanda vya EPZ.

Kamanda wa polisi eneo la Pwani Noah Mwivanda alisema polisi wanawalenga raia wa Pakistani wapatao 163 wanaofanya kazi katika viwanda mbali mbali kaunti ya Mombasa.

Bw Mwivanda alisema msako huo umepamba moto eneo la Pwani hususan kwenye sekta ya hoteli ambayo ni kitega uchumi kwa taifa hili.

“Tunanuia kuhakikisha tunawaregesha makwao raia wa kigeni wanaofanya kazi humu nchini bila vibali kwani tumepata habari kuwa hawa watu huja humu nchini kufanya kazi na kukwama huku baada ya muda walioruhusiwa kukamilika,” akasema Mwivanda.

“Upelelezi wetu ulibaini kuwa kuna zaidi ya raia 163 wa Pakistani wanaofanya kazi kwenye viwanda vitatu Mombasa, nimeagiza wakamatwe na kuregeshwa makwao.”

Afisa huyo alisema msako huo utafanywa kaunti zote za pwani ili kuhakikisha raia wote wa kigeni wanaoishi humo kwa njia haramu wanatimuliwa.

Msimamizi wa Chama cha Wahudumu wa Mahoteli na Wapishi (KAHC) Sam Ikwaye, alikiri kuwa kuna raia wengi wa kigeni wanaohudumu kwenye sekta hiyo bila vibali.

“Wengi wamo kwenye vyumba malaalum vya kukodi na tuko tayari kusaidia polisi,” akasema Bw Ikwaye.

Serikali imerudisha makwao wawekezaji sita wa madini waliokuwa wamekamatwa na polisi mjini Voi, kaunti ya Taita Taveta wakifanya biashara ya vito kinyume na sheria.

Raia hao wa Sri Lanka ni miongoni mwa wengine 17 wa kigeni waliokamatwa katika kaunti hiyo kwa kuwa nchini bila stakabadhi.

Awali, wawekezaji hao ambao walikuwa wakizuiliwa katika kituo cha polisi cha Voi walidai kuwa kushikwa kwao kulikiuka sharia, lakini wakasafirishwa na idara ya uhamiaji.