Mchoraji vibonzo wa ‘Taifa Leo’ ang’aa

Mchoraji vibonzo wa ‘Taifa Leo’ ang’aa

Na MARY WANGARI

MCHORAJI vibonzo wa Taifa Leo, Samuel Muigai, almaarufu Igah, ameibuka mshindi katika tamasha la kimataifa kuhusu uchoraji vibonzo, lililoandaliwa na Ubalozi wa Iran.

Igah alijinyakulia nambari 128 katika shindano hilo kwa jina World Cartoon Festival on Applying Arts and Culture in Silencing the Guns in Africa, lililojumuisha washiriki 687 kutoka duniani kote.

Aliwaongoza Wakenya wenzake wawili Edwin Erick Njue na Andala Bonface Okumu, walioshikilia nambari 194 na 205 mtawalia.

Mchoraji vibonzo wa Brazil, Cau Gomez aliibuka wa kwanza duniani katika shindano hilo akifuatiwa na Ares wa Cuba na Michel Moro Gomez wa Iran, walioorodheshwa katika nafasi ya pili na ya tatu mtawalia.

Tuzo hizo zilifanyika Nairobi mapema wiki hii wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Kimataifa kuhusu Amani na Majadiliano.

Balozi wa Iran Jafar Barmaki, alisema japo bunduki zimeundwa kwa lengo la kulinda maisha, zinaweza zikageuka ghafla kuwa hatari na zenye uharibifu, zinapoishia kwa watu wasiofaa jinsi inavyoshuhudiwa ulimwenguni.

Alifafanua kiwa tamasha hilo lililoandaliwa kwa ushirikiano na Umoja wa Afrika kupigia debe utamaduni wa Afrika pamoja na mradi wa “Kunyamazisha Bunduki.”

“Katika Tamasha letu, wasanii wengi kutoka ulimwenguni kote walithibitisha ari yao ya kuelezea jumbe za dhati zinazoambatana na kaulimbiu yetu ambayo ni kunyamazisha bunduki Afrika,” alisema kupitia taarifa iliyoonekana na Taifa Leo.

“Maelfu ya watu hufariki kila siku kutokana na majeraha ya risasi, huku wengine zaidi wakiachwa na majeraha mabaya. Ikiwa vifo, majeraha na ulemavu kutokana na silaha vingeorodheshwa kama ugonjwa, vingehitimu kuwa janga. Lakini vyombo vya habari na mtazamo wa wengi huashiria kuwa ukatili wa bunduki ni matokeo tu yasiyoweza kuepukika ya ukatili wa binadamu au ukosefu, badala ya tatizo la afya ya jamii linaloweza kuzuiwa au angalau kupunguzwa,” alisema.

You can share this post!

CBC: Kuppet pia wana malalamishi

Polisi waanza kufanya uchunguzi baada ya moto kuchoma...