Michezo

Mchuano wa Kenya dhidi ya Misri U-20 wafutwa

March 16th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MECHI za kirafiki kati ya timu ya soka ya Kenya na Misri ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20 ya wanaume, zimefutiliwa mbali.

Taarifa kutoka Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) imesema Ijumaa mechi hizo zilizopangiwa kusakatwa nchini Kenya na Misri mnamo Machi 24 na Machi 27 hazitaendelea jinsi zilivyopangwa.

Hata hivyo, FKF haitangaza sababu ya michuano hiyo kutolewa.

Hatua hii inaweka Kenya katika hatari ya kutojipima nguvu dhidi ya timu ya taifa kabla ya kumenyana na Rwanda baadaye mwezi huu katika mechi ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika la Under-20 nchini Niger mwaka 2019.

Timu hii ya Kenya iliratibiwa kulimana na Tanzania katika mechi ya kirafiki wiki chache zilizopita jijini Dar es Salaam, lakini pia ikafutiliwa mbali bila sababu kutolewa.

Licha ya mechi hizo kuondolewa, Kenya inasalia kambini uwanjani Kasarani kujinoa kabla ya kibarua kigumu dhidi ya Rwanda.