Mchujo wa UDA utaendeshwa kwa njia huru na haki, Ruto asema

Mchujo wa UDA utaendeshwa kwa njia huru na haki, Ruto asema

 Na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto amewahakikishia wale wanaotaka kuwania nyadhifa mbalimbali katika uchaguzi mkuu ujao kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) kuwa mchujo wa chama hicho utaendeshwa kwa njia huru, haki na itakayokubalika.

Alisema amejitolea kukiimarisha chama hicho kuwa chenye sura ya kitaifa na kitakacholeta umoja, utawala bora na maendeleo nchini kwa kipindi kirefu.

“Tunajenga chama kikubwa kitakachomilikiwa na wananchi. Hii ndio maana tumejitolea kuhakikisha kuwa uteuzi wetu wa wagombeaji unaendeshwa kwa njia huru itakatokubalika na washiriki wote. Tunataka kushuhudia hali ambapo watakaopoteza katika mchunjo wanawaunga mkono wale watakaoshinda ili kwa pamoja kuiwezesha UDA.

“Katika mchujo wa UDA watu wote watakuwa washindi. Hakuna atakayeshindwa. Wale watakaoshindwa watajumuishwa kwenye orodha ya watakaoteuliwa kuhudumu kama wabunge na madiwani maalum,” Dkt Ruto akakariri.

Naibu Rais alikuwa akizungumza katika makazi yake rasmi katika makazi yake rasmi mtaani Karen, Nairobi alipokutana na jumla ya wagombeaji 600 wa viti mbalimbali, kwa tiketi ya UDA, kaunti ya Nairobi.

Viongozi waliohudhuria mkutano huo walikuwa Gavana wa Turkana Josphat Nanok, Senata Millicen Omanga na wabunge; James Gakuya (Embakasi Kaskazini), Benjamin Gathiru (Embakasi ya Kati), John Kiarie (Dagoretti Kusini), George Theuri (Embakasi Magharibi) Rigathi Gachagua (Mathira), Nixon Korir (Lang’ata), Alice Wahome (Kandara) na John Wanjiku (Kiambaa).

Dkt Ruto alisema chama cha UDA kitabadilisha mkondo wa siasa nchini kwa “kuiondoa kutoka kwa meno ya ukabila na kuanzisha mjadala kuhusu ukuzaji wa kiuchumi.”

“Tunalenga kujenga nchi ambayo inatoa nafasi sawa kwa wote. Katika UDA, ufanisi wenu utatokana na bidii yenu na kujitolea kwenu, wala sio yule unayemfahamu,” akasema.

Katibu Mkuu wa UDA Veronica Maina alisema chama hicho kitafanya kazi na viongozi wote na huku ikishauriana na wagombeaji wote wa viti vya kisiasa.

“Hakutakuwa na njia mkato katika UDA. Matokeo ya mchujo yataamuliwa na wapiga kura,” akasema.

Kumekuwa na hofu miongoni mwa nwandani wa Dkt Ruto kwamba huenda mchujo wa UDA hautaendeshwa kwa njia huru na haki.

Hii ndio baada baadhi ya wanasiasa walioko katika mrengo wa Tangatanga kama vile Moses Kuria na aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri wamekataa kuvunja vyama vyao ili kujiunga na UDA kama wanachama wa moja kwa moja.

You can share this post!

Celtic wakung’uta AZ Alkmaar kwenye mchujo wa Europa...

Linda Katiba wasema waliopendekezwa kuteuliwa makamishna wa...