Dimba

Mchumba wa Jorginho amkingia kuhusu tuhuma za kujituma chumbani kuliko kambini Arsenal

May 11th, 2024 2 min read

NA CHRIS ADUNGO

CATHERINE Harding, ambaye ni mchumba wa kiungo Jorge Luiz Frello almaarufu Jorginho alitumia chapisho la video mitandaoni kucharukia watu wenye mazoea ya kukashifu mumewe kwa “kupenda vya chumbani kupindukia kuliko jinsi anavyojituma uwanjani.”

Licha ya kukashifiwa na mahasimu kila anapokosa kutamba ugani, Jorginho, 32, amekuwa tegemeo kubwa kambini mwa Arsenal katika kipindi chote ambapo Thomas Partey alikuwa akiuguza jeraha.

Kwa mujibu wa wakosoaji, “Jorginho anapenda sana miereka ya siri kiasi kwamba mkewe amekuwa akitumia mitandao ya kijamii kujigamba kuhusu ujogoo wake chumbani.”

Hivi majuzi, Catherine alipakia kwenye Instagram video iliyorekodiwa akimsifu Jorginho huku akitamani arejee nyumbani upesi kumburudisha chumbani baada ya mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyoshuhudia Arsenal wakipigwa 2-0 na Aston Villa ugani Emirates.

Haikuwa mara ya kwanza kwa mwimbaji huyo kuingia Instagram kujinaki na kutangazia mashabiki jinsi anavyotoshelezwa kimapenzi na Jorginho. Wiki hii, aliwakemea wakosoaji wa mume wake kwenye chapisho refu aliloambatanisha na wimbo wa Abba wa ‘Money, Money, Money’.

Catherine alisema: “Nimekuwa nikiona maoni mengi kuhusu Jorginho mitandaoni ila nimekuwa nikipuuza. Lakini leo nimepata ujasiri wa kuwapasha.”

“Hivi mumeliona dume langu? Ni jamaa mtanashati sana na amebarikiwa sana! Huwa ni raha na shangwe tele kila ninapokuwa naye chumbani. Wenye wivu komeni kabisa na wala msifikirie kwamba mnaweza kupata fursa ya kumwonjesha chochote!”

“Mume wangu anapendeza siku zote na inapendeza sana kuwa naye maana tunaweza kucheka siku nzima pamoja bila kufanya chochote. Pia ana nguvu za ndovu na ni tajiri wa ‘mali’. Yeye si mchezo katika mchezo wa chumbani’. Sidhani kuna aliye na bahati kubwa zaidi yangu.”

Jorginho alimvisha Catherine pete ya uchumba mwishoni mwa mwaka jana na kulikoleza kabisa penzi lao. Nyota huyo alianza kudokoa tunda la kichuna huyo mnamo 2020, muda mfupi baada ya kutemana na aliyekuwa mkewe, Natalia.

Ndoa yake na Natalia ilidumu kwa miaka miwili na ikajaliwa mtoto wa kiume anayeitwa Jax. Hadi alipojipa kwa Jorginho, Catherine, ambaye ni mwanamuziki maarufu raia wa Ireland, alikuwa akitoka kimapenzi na Jude Law.

Uhusiano wake na mwigizaji huyo maarufu wa Hollywood ulijaliwa mtoto wa kike.