Habari Mseto

Mchungaji hali mahututi baada ya kuvamiwa na fisi

February 24th, 2019 1 min read

NA CHARLES WANYORO

MWANAUME mwenye umri wa miaka 54, kutoka Kaunti ya Marsabit, amelazwa katika hospitali ya Kenyatta akiwa katika hali mahututi, baada ya kuvamiwa na fisi mnamo Ijumaa.

Lepati Saidinga, alikumbana na mnyama huyo aliyemjeruhi kwenye meno na kuuma mboni ya jicho lake, punde tu alipokamilisha kuwapa mifugo wake maji na kuinama kunawa uso wake.

Fisi huyo pia aliuma vidole vyake vitatu kwenye mkono wake wa kulia, akajeruhi miguu yake na kumwacha na majeraha mabaya katika mkono wake wa kushoto. Kando na hayo, mnyama huyo wa mwituni alimng’oa meno mawili na kurarua jicho lake na pua.

Rafikiye, Lesapuk Namarti, 27, aliyefika kumwokoa, pia hakusazwa na fisi huyo alipomuuma kwenye mkono wa kushoto na miguu. Hata hivyo alipiga nduru na wachungaji wenzake wakafika kuwaowokoa kisha wakamuua mnyama huyo.

Msimamizi wa kitengo cha uuguzi katika hospitali ya Kenyatta, Yusuf Galmoge amesema Bw Saidinga alifikishwa humo akiwa hali mahututi na alifanyiwa upasuaji Jumamosi.

Bw Namarti naye amelazwa katika hospitali ya kaunti ndogo ya Laisamis, lakini madaktari hospitalini humo wamesema hayuko katika hali ya hatari.