Makala

Mchuuza maji sasa amiliki chuo cha urembo

July 25th, 2020 3 min read

Na SAMMY WAWERU

Ukiuliza Samuel Karanja matunda, mazao au zawadi ya kutia bidii maishani, atakujibu bila kusita na kukupa motisha “hakuna hali inayoota mizizi”.

Licha ya changamoto kibao alizokumbana nazo awali, wakati akipalilia msingi wa talanta yake, Karanja sasa ni msusi hodari wa kupigiwa upatu.

Ufanisi wake, ni historia inayoweza kusimuliwa kwa muda wa siku kadhaa, ila katika maandishi anaifupisha.

Mwaka 2014, Karanja aligura masomo kwa sababu ya ukosefu wa karo. Alikuwa kidato cha pili mwaka huo.

Ulikuwa uamuzi chungu kufanya, sawa na kumeza tembe shubiri na hakuwa na budi ila kuzika katika kaburi la sahau ndoto yake ya muda mrefu kuwa mwalimu.

Aidha, anasema alianza safari kujiendeleza kimaisha, kukimu mahitaji yake ya kimsingi. “Nilianza kwa kuchuuza njugu karanga na maji ya chupa za plastiki. Pia, nilifanya kazi ya kuosha magari Nairobi,” Karanja ambaye ni mzaliwa wa Kiambu anafichua. Ulikuwa mwaka wa 2015 wakati huo.

Kijana huyu anasema muda ulivyozidi kusonga alivutiwa na shughuli za kurembesha kina dada, ambapo alianza kwa kunakshisha kucha zao kwa hina, rangi tofauti na pia kuzinadhifisha.

Ni kazi ya sanaa inayohitaji mikono, macho na akili kama ‘zana’ za kazi, na alichohitaji ni mapenzi, vifaa na ubunifu.

Kulingana na Karanja, 25, pia alivutiwa na ususi. “Mtaji kidogo niliokuwa nimeweka kama akiba nilijiunga na taasisi moja inayotoa mafunzo ya ususi wa nywele na urembesho wa wanawake jijini Nairobi,” anaeleza mjasirimali huyu anayemiliki duka la kisasa kufanya ususi na kurembesha kina dada, saluni, eneo la Zimmerman, Nairobi.

Anasema wazazi wake walimtaka asomee kozi ya kiufundi, hasa umekanika huku wakipuuzilia mbali ususi walioutaja “ni kazi ya jinsia ya kike”.

Dhana kuwa ni kazi ya jinsia ya kike, haikumbabaisha kamwe. Miezi kadhaa baadaye, alifuzu akiwa amejihami na ujuzi na maarifa, Karanja akidokeza alianza kama msusi tamba.

Anafichua kwamba alianza kwa mtaji wa Sh200 pekee. “Kutoa huduma za ususi na kurembesha wateja katika makazi yao haikuwa jambo rahisi. Baadhi hawakufurahia nyumba zao kuingiwa, hususan waume wao,” Karanja akaambia Taifa Leo Dijitali wakati wa mahojiano.

Isitoshe, alisema “kuna walioahirisha kuhudumiwa dakika za mwisho wakati ambapo amepangua ratiba ya wengine waliomhitaji”.

Kufikia mwaka wa 2017, Karanja anasema alikuwa ameweka kibindoni akiba ya Sh50, 000, fedha alizotumia kufungua saluni Nairobi. Baadaye, aliimarisha utendakazi na kupanua ikawa ya kisasa, hatua iliyomgharimu takriban Sh500, 000.

Akiorodheshwa katika listi ya wawekezaji wachanga, Karanja pia ana chuo cha mafunzo ya ususi na kurembesha na kunakshisha wanawake eneo la Githunguri, Kaunti ya Kiambu, hatua anayoisifia imemfanya kuwa mmoja wa mmiliki wa taasisi za elimu ya juu nchini.

“Ufanisi wangu umejiri kwa neema ya Mwenyezi Mungu. Nikifingua chuo kilichonigharimu zaidi ya Sh250, 000, ilinikumbusha wakati mmoja nilitamani kuwa mwalimu,” Karanja anaelezea.

Kati ya miundo na staili za nywele anazosuka ni pamoja na twist braids, lines, crochet stitch, bandika dreads, weaving na wigs, miongoni mwa zingine.

Huduma anazotoa ni gel na tips, retouch, pedicure, manicure, nail polish, hair treatment na blow-dry. Malipo yake ni kati ya Sh100 – 2, 500.

Licha ya jitihada zake, mkurupuko wa Covid – 19 nchini, ugonjwa ambao sasa ni kero la kimataifa na unaosababishwa na virusi vya corona, nusra uzime ndoto zake.

Wakati wa mahojiano, Karanja alisema tangu Kenya ithibitishe kisa cha kwanza cha corona, biashara yake imeathirika.

Kuzuia msambao wa Covid – 19, serikali kupitia Wziara ya Afya ilitoa mwongozo, wenye mikakati inayodhibiti mkusanyiko wa watu.

Hali kadhalika, serikali iliagiza shule, vyuo na taasisi zote za elimu nchini kufungwa. Karanja anasema hakuwa na budi ila kutii amri hiyo, akieleza kwamba analipia majengo yanayositiri chuo chake cha mafunzo ya ususi na urembesho.

Wizara ya Elimu imetangaza kuwa shule, vyuo na taasisi za elimu nchini zitafunguliwa mapema mwaka ujao 2021.

Karanja pia anasema shughuli zake za ususi na kurembesha zimeathirika, ambapo amepunguza idadi ya wafanyakazi kutoka 15 hadi 5. “Ili kuzingatia kigezo cha umbali kati ya mtu na mwenzake, nilipunguza kiwango cha wafanyakazi,” anasema.

Kabla Kenya kuwa mwenyeji wa janga la corona, anasema saluni yake ilisheheni shughuli chungu nzima kuhudumia wateja. Anasema awali kwa siku alikuwa akipokea kati ya wateja 20 – 30, na kutokana na athari za Covid – 19 wamepungua kwa kiasi kikuu, akidoza kwamba hawazidi wanane.

Mwanasanaa huyu anafafanua kuwa kwa sasa anatoa huduma kupitia oda. “Tunafanya kazi kwa oda, wateja wanauliza kwa njia ya simu ili kuepuka kukusanyika au kusongamana kwenye saluni,” anaeleza, akiongeza kusema kuwa iwapo oda hazipo kazi haifunguliwi.

Ni kutokana na athari za corona ambapo Karanja amelazimika kutathmini malipo ya huduma zake, kwa kupunguza kati ya Sh200 – 300 ili kuvutia wateja.

Sawa na msusi huyo, Lilian Wambui ambaye ameajiriwa anasema kwa siku anahudumia wateja wasiozidi watatu, ikizingatiwa kuwa analipwa kulingana na idadi ya wateja. “Malipo ni kati ya asilimia 30 – 50 kwa kila mteja ninayehudumia. Maisha yanazidi kuwa magumu,” Wambui anasema.

Samuel Karanja anasema awali alikuwa akipokea faida isiyopungua Sh40, 000 kwa mwezi, baada ya kuondoa gharama ya matumizi kama vile leba – ndiyo mishahara ya wafanyakazi na kodi ya saluni, miongoni mwa matumizi mengine.

Alikuwa akifanya kazi hadi saa sita za usiku, ila sasa ifikapo saa mbili za jioni anafunga ili kuafiki amri ya kafyu ya kitaifa inayotekelezwa kati ya saa tatu usiku hadi saa kumi alfajiri.

Karanja anatumia mitandao ya kijamii kama vile Facebook, WhatsApp na pia Instagram kupigia upatu huduma zake.

Covid – 19 ni janga la kimataifa na ambalo limeathiri sekta mbalimbali ulimwenguni, na licha ya changamoto zilizopo Karanja anasema hajafa moyo. “Ni janga la muda, ni jaribio tu la imani yetu. Tunamcha Mungu na tunatumai atatuondolea, tutaibuka washindi,” anaeleza, akipa wafanyabiashara motisha kutokata tamaa.