Habari Mseto

MCK kuanzisha msako dhidi ya wanahabari bandia

November 19th, 2018 1 min read

Na COLLINS OMULO

BARAZA la kusimamia sekta ya Uandishi wa Habari (MCK) limeelezea hofu yake kuhusu kuongezeka kwa watu wanaojifanya kuwa wanahabari, likisema litaanzisha msako mkubwa ili kuwakamata.

Afisa Mkuu Mtendaji (CEO) wa MCK David Omwoyo alisema kuwa baraza hilo linalenga kaunti sita ambazo zimeadhihirika zaidi, katika operesheni ambayo itaanzishwa ndani ya kipindi cha wiki moja.

Bw Omwoyo alisema kuwa wakora hao wamekuwa wakifanya makosa kama kuchapisha habari za uongo, kupokea rushwa na kuitisha pesa kutoka kwa watu wanaotaka kuchapisha habari.

Alisema katika Kaunti ya Kilifi pekee, visa 19 vimeripotiwa wiki chache zilizopita. Alisema kuwa MCK inalenga kaunti za Homa Bay, Nairobi, Kisumu, Mombasa, Turkana na Garissa kwa operesheni hiyo. Alisema baraza hilo linaandikia kaunti husika, akiahidi kuwa shughuli hiyo itafanywa kwa njia nzuri zaidi.

“Ni changamoto kuu. Tutavamia wakora wanaojifanya kuwa wanahabari kwa kuwa MCK ndilo shirika pekee lenye mamlaka ya kuwasajili wanahabari nchini. Hao wakora wanazunguka sehemu kwa sehemu wakiitisha pesa na kuchapisha habari za uongo,” Bw Omwoyo akasema.

Afisa huyo alikuwa akizungumza wakati wa kongamano la siku tano na waandishi wa habari, ambalo liliandaliwa na serikali ya Kaunti ya Nairobi katika hoteli ya English Point Marina, Mombasa, ambalo lilikamilika jana.

Bw Omwoyo, aidha alishauri pawepo ushirikiano mwema baina ya kaunti na waandishi wa habari ili kuzuia visa ambapo wanahabari wanadhulumiwa ama kunyimwa habari zenye umuhimu katika serikali za kaunti kwa kuwa tu “wameandika habari isiyofurahiwa.”

Alishauri wanahabari vilevile kuandika habari zaidi kuhusu maendeleo, akisema jukumu lao linasaidia sana katika kufahamisha umma na hivyo si vyema habari zote kuwa mbaya.

Gavana wa Nairobi Mike Sonko naye alirai wanahabari kuongeza idadi ya habari nzuri wanazoandika, akisema zinasaidia kuwapa motisha raia.

Maafisa zaidi ambao walihudhuria kongamano hilo walijadili masuala nyeti yanayoadhiri Kenya, wataalam wa uchumi na maafisa kutoka EACC pia wakishiriki.