Mdahalo: Wawaniaji ugavana wafafanulia wakazi wa Kiambu ajenda zao

Mdahalo: Wawaniaji ugavana wafafanulia wakazi wa Kiambu ajenda zao

NA LAWRENCE ONGARO

WAWANIAJI wanne wa kiti cha ugavana katika Kaunti ya Kiambu walihojiwa na kituo cha habari cha Citizen ambapo walipata fursa ya kufafanua ajenda zao kwa wakazi wa Kiambu.

Viongozi hao ni Bw William Kabogo wa chama cha Tujibebe Wakenya Party, Bw Patrick ‘Wajungle’ Wainaina (Mgombea wa Kujitegemea), Kimani Wamatangi (UDA), na Bi Mwende Gatabaki (Safina).

Katika mjadala huo wawaniaji wawili hawakuhudhuria. Wawili hao ni Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro (Jubilee), na Moses Kuria (Chama cha Kazi).

Kwenye mjadala huo, Kabogo alisema rekodi yake ya kuinua sekta ya afya bado inakumbukwa na wakazi wa Kiambu ambapo hata wakati huu watu wanasikikika mara kwa mara wakisema maneno kama “Kaba Kabogo” yaami “Afadhali Kabogo.”

Aliahidi kwamba endapo atachaguliwa atazidi kuimarisha sekta ya afya.

Alisema wakati wa uongozi wake kama gavana, aliweka mipangilio bora ambayo inaendelea kuigwa hadi wakati huu.

Naye mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Wajungle’ Wainaina katika mjadala huo alisema yeye kama mbunge amefanya mengi kama kujenga miundomsingi, kuboresha sekta ya kilimo, kukarabati shule za msingi na za upili na pia kuinua wengi kiuchumi.

Alisema iwapo atapewa nafasi hiyo, atahakikisha anaendeleza mambo hayo yote bila kubagua.

“Mimi nikichaguliwa nitakuwa mtumishi wa watu wa Kiambu ambapo watapata maendeleo hadi mashinani,” alijitetea Bw ‘Wajungle’.

Bw Wamatangi ambaye ndiye Seneta wa kaunti ya Kiambu, alisema kaunti hiyo imepoteza mabilioni ya fedha kupitia ufisadi na kwa hivyo akipata nafasi hiyo, atafanya juhudi kuona ya kwamba fedha za umma zinalindwa kikamilifu.

Alisema fedha zinazopelekwa kaunti ya Kiambu zinastahili kutumiwa kwa umakini ili kunufaisha kila mkazi.

Naye Bi Gatabaki alisema “inashangaza sana kuwaona walevi wengi katika kaunti hii ya Kiambu.”

“Hiyo haimaanishi eti hawana pesa bali wamejiingiza kwa hali hii kutokana na matatizo mengi wanayopitia. Bila shaka watu wa aina hiyo wanastahili kupewa mwongozo ili washughulikie maswala muhimu ya kuimarisha maisha,” alifafanua Bi Gatabaki.

Alisema kunastahili kuwepo mpangilio maalum wa kushughulika matatizo yanayokumba wakazi wa Kiambu.

Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro katika kampeni zake za hivi majuzi alieleza kuwa kwa muda wa miaka miwili amezindua miradi kadha hasa ya miundomsingi, afya, maji na elimu.

Kwa hivyo aliwarai wakazi wa Kiambu wadadisi viongozi kwa makini kabla ya kuwapa nafasi ya uongozi.

  • Tags

You can share this post!

Polisi waanza uchunguzi baada ya ofisi ya ‘Jicho Pevu’...

PAA sasa yamezwa na Kenya Kwanza, yashindwa kupaa

T L