MDC yabadili jina kukabili vikwazo

MDC yabadili jina kukabili vikwazo

Na KITSEPILE NYATHI

HARARE, ZIMBABWE

CHAMA kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe kimebadilisha jina lake ili kushinda changamoto ya kisheria na misukosuko ndani yake, iliyotishia kukisambaratisha kabla ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Machi.

Chama cha Muungano wa Movement for Democratic Change (MDC), kilichobuniwa mnamo 1999, Jumatatu kilisema kuwa sasa kitajulikana kama Citizens Coalition for Change (CCC).Kiongozi wa chama hicho, Nelson Chamisa, Jumanne aliambia wanahabari jijini Harare kwamba jina, alama na rangi za MDC zilibadilishwa kuzuia jaribio la serikali ya Rais Emmerson Mnangagwa kukinyima nafasi ya kuendesha shughuli zake.

“Sisi ni nambari moja nchini. Mabingwa wanapigwa vita na wale ambao hawana nguvu. Huwezi kutushinda. Mipango yetu ya kupata sura na jina jipya imekamilika,” akasema Bw Chamisa, 43, ambaye alishindwa kwa kura chache na Rais Mnangagwa katika uchaguzi mkuu wa 2018.

“Wananchi wapewe nafasi kuu. Mtu mmoja kura moja…. Haitakuwa rahisi. Wananchi huendesha magurudumu ya taifa. Kila raia wa Zimbabwe sharti ajiandae kwa mabadiliko.”

Muungano wa MDC umepitia wakati mgumu katika uchaguzi mkuu wa 2018.

Kwa mfano mnamo 2019 Mahakama ya Juu iliamua kwamba uchaguzi wa Bw Chamisa kuwa kiongozi wa chama hicho baada ya kifo cha mwanzilishi wake Morgan Tsvangirai, ulifanywa kinyume cha sheria.

Mrengo wa chama hicho uliopinga uchaguzi wa Bw Chamisa, uliruhusiwa kuondoa wabunge wake na wawakilishi wake katika serikali za wilaya.

Chama hicho pia kilipoteza mali, ikiwemo makao yake makuu huku serikali ikikataa kutoa mgao wake wa fedha ambazo hutolewa kwa vyama vinavyowakilishwa bungeni.

Rais Mnangagwa alikashifiwa kwa kujaribu kurejesha utawala wa chama kimoja kwa kuhujumu chama kikuu cha upinzani.Hata hivyo, Muungano wa MDC unasema juhudi hizo zimefeli na kuapa kukishinda chama tawala Zanu PF katika chaguzi za ubunge na udiwani zitakazofanyika Machi 26, 2022.

Itakuwa ni mara ya kwanza kwa Zimbabwe kufanya chaguzi baada ya shughuli hizo kupigwa marufuku miaka miwili iliyopita kufuatia mlipuko wa ugonjwa hatari wa Covid-19.

“Zimbabwe mpya imezaliwa. Tuko hapa na tumepata chombo kipya na mipango mipya. Nimeachana na yale ya zamani,” Bw Chamisa akasema.

“Tunawakilisha matumaini mapya, furaha na uhuru. Tunawakilisha mawazo mapya ambayo yanakumbatiwa na raia wote. Tumepoteza kila kitu isipokuwa nafsi zetu. Ukitaka MDC Alliance, ichukue. Hatuwezi tukauzwa,” mwanasiasa huyo akasema akionekana kumwambia Rais Mnangagwa.

Bw Chamisa alisema wamejitolea kuleta mabadiliko nchini Zimbabwe na “hatutatishika. Tutaendelea na mipango yetu bila uwoga.”

Alisema chaguzi za ubunge na udiwani ni hatua ya kwanza kuelekea uchaguzi mkuu 2023 ambapo Rais Mnangagwa atatafuta nafasi ya kuongoza kwa muhula wa pili.

Rais Mnangagwa alichukua hatamu za uongozi wa Zimbabwe baada ya kuondolewa mamlakani kwa rais wa zamani marehemu Robert Mugabe.

Dkt Mugabe aliondolewa katika mapinduzi yaliyotekelezwa na wanajeshi.

Hata hivyo, Rais wa sasa Bw Mnangagwa analaumiwa kwa kushindwa kutimiza ahadi ya kurejeshwa uongozi wa kidemokrasia nchini Zimbabwe.

  • Tags

You can share this post!

Watu 32 wauawa katika shambulio jimboni Jonglei

Tangatanga wavuruga hoja ya kuunda kamati ya bajeti

T L