Michezo

Mechi 10 kugaragazwa Jumatamo NSL

October 14th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

JUMLA ya michezo 10 imeratibiwa kugaragazwa Jumatano hii kwenye kampeni za kufukuzia ubingwa wa Supa Ligi ya Taifa (NSL) muhula huu.

Viongozi wa kipute hicho, Nairobi City Stars watatifua vumbi dhidi ya mahasimu wao Nairobi Stima kwenye patashika inayopigiwa chapuo kuzua msisimko wa kufa mtu itakayopigiwa uwanjani Ruaraka, Nairobi.

City Stars ya kocha, Sanjin Alagic itashuka dimbani ikijivunia kunyamazisha Maafande wa APs Bomet kwa bao 1-0 nayo Nairobi Stima iliandikisha ufanisi wa goli 1-0 mbele ya FC Talanta wiki iliyopita.

City Stars imeorodheshwa miongoni mwa vikosi vinavyotetemesha wapinzani wao kwenye kampeni za kipute hicho msimu huu.

Baada ya mafanikio hayo naibu kocha wa City Stars, John Amboko alinukulia akisema, ”Tunapania kupigana kwa udi na uvumba kuhakikisha tunasa tiketi ya kupandishwa daraja kushiriki Ligi Kuu ya KPL muhula ujao.”

Wanasoka wa City Stars wanaongoza kwenye jedwali la mechi hizo kwa kuzoa alama 22, tano mbele ya Nairobi Stima. Nayo Bidco United na Vihiga United zitaingia mjegoni kucheza dhidi ya Kibera Black Stars (KBS) na Shabana FC mtawalia.

Baada ya Ushuru FC kulimwa mabao 2-1 na Mt Kenya wiki iliyopita, Jumatano hii itakabili Vihiga Bullets.

Katika ratiba hiyo, APs Bomet itavana na Murang’a Seal, FC Talanta itapambana na Fortune Sacco nayo Mt Kenya itakutanishwa na Migori Youth.

Nao washiriki wapya, North Wanderers ambao wamedondosha mechi zote nane wavaana na St Joseph’s Youth, Administration Police itaingia katika ardhi ya nyumbani kukwaruzana na Modern Coast Rangers