Michezo

Mechi isiyotabirika ‘Sauzi’ na Cape Verde zikikabana koo robo fainali Afcon

February 3rd, 2024 1 min read

JOHN ASHIHUNDU NA MASHIRIKA

AFRIKA Kusini inapewa nafasi kubwa ya kushinda Cape Verde Jumamosi usiku na kufuzu kwa nusu-fainali ya fainali za Kombe la Mataifa Bora barani Afrika (Afcon), lakini haitakuwa rahisi jinsi mashabiki wengi wanavyofikiria.

Cape Verde ilishinda Mauritania 1-0 katika pambano la raundi ya 16-Bora na kufuzu kwa robo-fainali ya michuano hii, hii ikiwa mara yao ya pili katika historia yao lakini kuna baadhi ya mashabiki wanaodai timu hiyo ilifuzu kichupuchupu.

Tayari kocha Pedro Bubista amesisitiza kwamba kiwango cha vijana wake kimemridhisha, huku akieleza matumaini makubwa ya kikosi hicho kubwaga Afrika Kusini na kusonga mbele.

Itakumbukwa kwamba mashabiki walishuhudia Cape Verde ikimaliza ya kileleni mwa Kundi A, mbele ya Nigeria ambao ni vigogo wanaofahamika, kando na kuorodheshwa katika nafasi nzuri kwenye viwango vya Fifa.

“Tumepiga hatua kubwa katika mashindano haya na tunajua upinzani mkali tutakaopata dhidi ya Afrika Kusini, lakini hatuogopi,” alisema kocha aliyeongeza kwamba vijana wake wamejiandaa vya kutosha kwa pambano hili.

Bubista alisema hayo baada ya kuona Afrika Kusini wakicheza kwa kiwango cha juu, hasa walipocheza na Morocco katika hatua ya 16-Bora na kushinda 2-0.

Afrika Kusini inayojivunia mastaa wanane kutoka klabu ya Mamelodi Sundowns wanatarajiwa kushinda mechi hii ikiwa watacheza kwa bidi jinsi walivyocheza dhidi ya Morocco ambao wanaorodheshwa katika nafasi ya 13 Duniani.

Safu ya ulinzi ya kikosi hicho inayojumuisha kipa Ronwen Williams, Khuliso Mudau, Mothobi Mvala, Aubrey Modiba na Grant Kekana imesifiwa baada ya kutofungwa bao katika mechi tatu mfululizo.