Michezo

Mechi nane kuchezwa wikendi ligi ya KYSD

September 27th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

JUMLA ya mechi nane zimepangwa kuchezwa wikendi hii kwenye kampeni za Ligi ya KYSD kwa wasiozidi umri wa miaka 14 zitakazopigiwa uwanjani KYSD Kamukunji, Nairobi.

Mabingwa watetezi Kinyago United wanapigiwa chapuo kufanya kweli watakapokabili Pro Soccer Academy Jumapili.

Nayo Volcano inayokuja kwa kasi kwenye michezo ya msimu huu imeratibiwa kuvaana na Young Elephants huku ikitazamiwa kutifua vumbi kali na kuzoa alama tatu muhimu.

Young Elephants itakuwa na mtihani mgumu kwenye patashika hiyo huku ikiumiza majeraha baada ya kulazwa magoli 5-2 na Lehmans wiki iliyopita.

Aidha Volcano itakuwa mbioni kulipiza kisasi baada ya kukubali kulala kwa mabao 3-2 mbele ya Fearless FC wiki iliyopita.

”Kama kawaida tumepania kushuka dimbani kushiriki mchezo huo kama fainali lengo letu likiwa kutesa wapinzani wetu bila huruma na kubeba ufanisi wa alama zote,” alisema nahodha wa Kinyago, Samuel Ndonye na kuongeza kuwa hawatalaza damu maana wakiteleza tu huenda wakajipata njiapanda kwenye kampeni hizo.

Kwenye ratiba ya Jumamosi hii, Pumwani Ajax itacheza na Fearless FC, Lehmans italimana na Young Achievers, Tico Raiders itapepetana na Gravo Legends nayo MASA itatifua vumbi dhidi ya Fearless Academy.

Kwenye ratiba ya Jumapili, Pumwani Foundation itamenyana na State Rangers huku Locomotive ikiumana na Sharp Boys.