Michezo

Mechi nane za Super Eight kuchezwa wikendi

March 21st, 2019 2 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

MICHUANO ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Super Eight itaendelea wikendi hii ambayo inabisha huku kukiwa na mechi nane katika viwanja mbali mbali.

Timu za Ng’ando Youth Association (NYSA) na Makadara Junior zitakuwa zikiwania ushindi wa kwanza wakati mechi hizo zimeingia wiki ya tatu.

NYSA watakuwa nyumbani Jumapili kuikaribisha Makadara Junior League SA katika mechi itakayochezewa Ngong Posta.

Baada ya kukosa kupata ushindi katika mechi mbili zilizopita, mashabiki wanatarajia timu zote kuingia uwanjani kwa vishindo.

NYSA ambao walimaliza katika nafasi ya nne msimu uliopita, wanajivunia pointi moja kutokana na sare ya 1-1 dhidi ya Githurai All-Stars kwenye mechi yao ya utangulizi. Kichapo cha 1-0 walichopokea kutoka kwa Shauri Moyo Sportiff wikendi iliyoipita kimewaacha katika nafasi ya 12, nafasi moja pekee mbele ya wapinzani wao.

Kihistoria, Makadara Junior wanapewa nafasi kubwa ya kuibuka washindi baada ya kuandikisha ushindi wa 2-1 kwa wapinzani msimu uliopita.

Hata hivyo, kocha wa NYSA, Fredrick Otieno amewaambia wageni wasitarajie kazi rahisi wakati huu.

“Huu ni msimu mpya na tumejiandaa vyema kuliko tulivyokuwa msimu uliopita. Yaliyotokea msimu uliopita tumeyasahau na tumeamua kuzua upinzani mkali,” alisema Otieno.

Kikosi imara

Kwa Makadara Junior, itabidi wapange kikosi imara baada ya kupoteza mechi za kwanza mbili dhidi ya Sportiff ya Githurai All-Stars mtawaliwa.

Kocha wao, Charles Achima amesema vijana wako makini baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo.

Kwingineko, Dagoretti Former Player FC watakuwa nyumbani ugani Riruta BP Stadium Jumampili kuvaana na Huruma Kona.

Mabingwa watetezi, Jericho All-Stars watakuwa ugenini kesho Jumamosi kucheza na Team Umeme katika mechi itakayochezewa Umeme Sports. Vijana hao kutoka Makadara wanatarajiwa kuendeleza ushindi wao baada ya majuzi kuitandika MASA 3-2.

TUK ambao wikendi iliyopita waliichapa Umeme 1-0 watakuwa ugani Ziwani kesho Jumamosi kupepetana na timu geni ya Lebanon FC.

Ratiba ya mechi za Jumamosi ni:

Githurai All Stars na Mathare Flames FC (Ruiru Sports Complex, saa tisa); Lebanon FC na TUK (Ziwani, saa saba); Kawangware United na Rongai All Stars (Riruta BP, saa tisa); Metro Sports FC na Shauri Moyo Sportiff (Drive Inn, saa tisa); MASA na Meltah Kabiria FC (Makongeni , saa tisa); Team Umeme na Jericho All Stars (Umeme Sports, saa tisa).

Mechi za Jumapili ni:

NYSA na Makadara Junior League SA (Ngong Posta, saa tisa); Dagoretti Former Players FC na Huruma Kona FC (Riruta BP Stadium, saa kumi).