Michezo

Mechi ngumu ya kutoa picha halisi ya mustakabali wa ‘Ndovu’ Arsenal

March 30th, 2024 2 min read

JOHN ASHIHUNDU Na MASHIRIKA

LIGI Kuu ya Uingereza (EPL) itafika hatua muhimu Jumapili jioni wakati Arsenal wanaoshikilia nafasi ya kwanza jedwalini watakuwa ugenini kukabiliana na wenyeji Manchester City ugani Etihad.

Mechi hii itakayoanza saa kumi na mbili na nusu jioni ni miongoni mwa chache zitakazotoa picha halisi kwenye vita vya kuwania ubingwa wa ligi hiyo maarufu.

Katika mechi nyingine ya Jumapili, Liverpool watakuwa nyumbani kualika Brighton katika pambano litakaloanza saa kumi kamili.

Baada ya kila mojawapo ya timu hizo kujibwaga uwanjani mara 28, Arsenal wako juu na pointi 64 wakifuatwa na Liverpool (64), Manchester City chini ya ukufunzi wa kocha Pep Guardiola wanakamata nafasi ya tatu kwa 63.

Arsenal na Man City ni mechi inayaotarajiwa kuzua upinzani mkali kwa sababu Arsenal wapo kwenye kiwango kizuri kwa sasa baada ya kushinda mechi nne zilizopita. Katika mkondo wa kwanza, Arsenal ilichapa City 1-0, bao lililofungwa na Gabriel Martinelli.

Guardiola ataunda kikosi chake bila John Stones na Kyle Walker walioumia wakichezea timu ya taifa ya Uingereza, lakini Manuel Akanji, Kevin de Bruyne na Matheus Nunes wanatarajiwa kuanza mechi hiyo.

Kwa upande mwingine, kocha Mikel Arteta anatarajia mastaa wake, Gabriel Jesus, Bukayo Saka na Martnelli kucheza, pamoja na kipa David Raya baada ya kukosa mechi yao iliyopita dhidi ya Brentford.

Manchester City wataingia uwanjani baada ya kutoshindwa nyumbani katika mechi 38 katika mashindano tofauti, wakishinda 33 na kutoka sare mara tano.

Kocha Guardiola ana rekodi nzuri dhidi ya Arsenal, ya ushindi mara 16, wakati huu Erling Haaland anajivunia mabao 11 katika mechi 16 akichezea City na timu ya taifa ya Norway katika mechi za kimataifa.

Arsenal ambao wameshinda mechi nane za EPL tangu mwaka 2024 uanze, wamefunga mabao 33 huku wakifungwa manne pekee, lakini watakuwa na kazi ya kuongeza pointi ili kujihakikishia kutimiza ndoto ya kutwaa taji hilo baada ya kusubiri kwa kipindi cha miaka 21.

Mshambuliaji wao Kai Havertz ni miongoni mwa wachezaji watakaotegemewa na Arteta baada ya Mjerumani huyo kufunga mabao manne katika mechi tano.

Mechi za leo zinachezwa wakati vita vya kusaka nafasi ya kushiriki michuano ya Klabu Bingwa (Uefa) na vile vya kushiriki Europa vikichacha.

Miongoni mwa mechi muhimu zitakazotoa picha halisi ni pambano kati ya Tottenham Hotspur na Manchester City, pamoja na ile kati ya Everton na Liverpool.

Baada ya mechi hii, City pia wana mechi nyingine muhimu dhidi ya Aston Villa itakayochezewa Etihad mnamo Aprili 3, 2024. Ugumu wa mechi hii ni kwamba wenyeji wanafukuzia ubingwa wakati Villa wakipigana kumaliza miongoni mwa Nne Bora. Villa ilishinda mkondo wa kwanza kwa 1-0.

Baada ya kumalizana na City, Arsenal watarejea uwanjani mnamo Aprili 6, 2024, kuvaana na Brighton ambayo pia inapigana vikali ikilenga kucheza katika michuano ya Ulaya msimu ujao.

Mechi nyingine muhimu itakuwa kati ya Manchester United na Liverpool ambao tayari wametupwa nje ya Kombe la FA na kuvuruga mpango wa kocha Jurgen Klopp kubeba mataji manne kwa mpigo.

Katika mechi nyingine muhimu, Arsenal itakuwa nyumbani Emirates kucheza na Aston Villa mnamo Aprili 14, 2024, kisha Tottenham dhidi ya Arsenal mnamo Aprili 27, 2024.

Pia Liverpool dhidi ya Tottenham mnamo Mei 4, 2024, na Astona Villa dhidi ya Liverpool hapo Mei 11, 2024, halafu Manchester United dhidi ya Arsenal, Mei 11, 2024, zitakuwa mechi tamu.

Arsenal, Liverpool na Manchester City zitakuwa nyumbani katika mechi zao za mwisho ambazo zitachezwa kwa wakati mmoja.