Michezo

Mechi saba wikendi hii ligi ya daraja la pili

November 2nd, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

MECHI saba zimeratibiwa kupigwa wikendi hii kwenye mfululizo wa kampeni za Kundi A Ligi ya Taifa Daraja la Pili.

Butterfly FC ya kocha, Bernard Shikuri inapigiwa upatu kuwasha moto mkali kusaka ushindi wa tatu itakaposhuka dimbani kukabili Ruiru Hotstars uwanjani Ruiru Stadium, mjini humo.

”Kama kawaida tutakuwa kazini tukilenga kuendeleza mtindo wa kutembeza vipigo dhidi ya wapinzani wetu msimu huu,” meneja wa Butterfly, Fredrick Ndinya alisema na kuongeza anatarajia kuona wachezaji wake wakijitahidi kwa udi na uvumba kupigania tiketi ya kufuzu kupandishwa daraja.

Kikosi hicho kimejaa furaha baada ya kushinda South B Sportiff wiki iliyopita. Butterfly FC ilifungua kampeni zake vyema kwa kukomoa Nanyuki Youth magoli 3-0.

Nayo Gogo Boys itakuwa ugenini kuvaana na washiriki wapya Utafiti FC uwanjani Kari Kikuyu.

Gogo Boys inayojivunia wachezaji wepesi kama Hillary Shirao na Kofa Taplah kati ya wengineo itakuwa mbioni kuwinda ushindi wa pili baada ya kulaza Korogocho Youth magoli 4-1 wiki iliyopita.

Kwenye mfululizo wa ratiba hiyo, Korogocho Youth itaalika CMS Allstars, Nyahururu Griffon FC itapepetana na South B Sportiff, Kibera United itakaribisha Kariobangi Sharks B nayo Tusker Youth itacheza na Vision FC katika uwanja wa Vision Mukuru Kwa Njenga, Embakasi.