Michezo

Mechi ya Gor, Homeboyz FC yapangwa upya

April 18th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MCHUANO wa kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) uliokuwa uwakutanishe Gor Mahia na Kakamega Homeboyz hii leo Alhamisi uwanjani Bukhungu, Kakamega umeratibiwa upya.

Kwa mujibu wa vinara wa KPL, kivumbi hicho kwa sasa kitatandazwa kesho kuanzia saa tisa alasiri katika uga uo huo wa Bukhungu.

Kiini cha kusogezwa kwa tarehe ya kupigwa kwa mchuano huo ni kucheleweshwa kwa safari ya Gor Mahia waliotarajiwa kurejea humu kutoka Morocco mnamo Jumanne.

Mabingwa hao mara 17 na watetezi wa taji la KPL walikuwa wageni wa RS Berkane ya Morocco katika marudiano ya Kombe la Mashirikisho barani Afrika (CAF).

Chini ya mkufunzi Hassan Oktay, Gor Mahia walibanduliwa kwenye kipute hicho baada ya kupokezwa kichapo cha jumla ya mabao 7-1.

Homeboyz ambao kwa sasa wananolewa na kocha Nicholas Muyoti, watashuka dimbani kuchuana na Gor Mahia wakijivunia hamasa ya kuwakomoa Vihiga United 1-0 katika mechi iliyowakutanisha wikendi jana.

Ushindi kwa Homeboyz utawapaisha hadi nafasi ya nne kwa alama 40, nne pekee nyuma ya Sofapaka ambao leo watachuana na Kariobangi Sharks.

Licha ya kusalia na michuano minne zaidi ya kucheza ili kufikia idadi ya mechi ambazo zimepigwa na wapinzani wao wakuu, Gor Mahia bado wamejidumisha pazuri jedwalini kwa alama 44 sawa na Sofapaka.

Wakati uo huo, mechi zote zitakazosakatwa na Chemelil Sugar pamoja na SoNy Sugar nyumbani kwao kwa sasa zitakuwa zinaanza saa saba mchana badala ya saa tisa alasiri.

Kwa mujibu wa waratibu, mabadiliko hayo yamechochewa na mvua kubwa ambayo kwa sasa inashuhudiwa katika maeneo hayo ya Chemelil na Awendo.

“Kipenga cha kuashiria mwanzo wa mechi zote zitakazopigwa na Chemelil na SoNy mbele ya mashabiki wao wa nyumbani sasa kitakuwa kikipulizwa saa saba. Hatua hii inalenga kupunguza uwezekano wa kuahirishwa kwa michuano inayihusisha vikosi hivyo kwa sababu ya mvua.”

Kwingineko, KPL wameratibu upya mchuano uliokuwa uwakutanishe Ulinzi Stars na Vihiga United mnamo Aprili 27 uwanjani Afraha, Nakuru.

Kipute hicho kwa sasa kitaandaliwa mnamo Aprili 24 ugani mumo humo.

“Mchuano kati ya Ulinzi Stars na Vihiga United kwa sasa utapigwa uwanjani Afraha mnamo Jumatano ya Aprili 24 badala ya Jumamosi ya Aprili 27 kama ilivyokuwa imeratibiwa awali.”

Mchuano huo utakuwa wa nane kwa wanajeshi wa Ulinzi Stars kushiriki chini ya kocha Benjamin Nyangweso aliyerejea mwezi jana kulijaza pengo la kocha Dunstan Nyaudo.

Ulinzi Stars na Vihiga United walikutana mara tatu mwaka 2018.

Walivaana mara mbili katika kampeni za KPL msimu uliopita kabla ya kupimana ubabe kwa mara nyingine katika mkondo wa kwanza wa kivumbi cha ligi muhula huu.

Jumla ya mabao matano yalifungwa katika mechi hizo tatu.