Michezo

Mechi za FKF Shield kurejelewa

September 18th, 2020 1 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

Michuano ya kuwania taji la FKF Shield iliyotibuka kutokana na maambukizi ya corona itarejelewa ili mshindi awakilishe Kenya katika michuano ya Confederation Cup, msimu ujao wa 2020/21.

Shirikisho la Kandanda Nchini (FKF) limesema mechi hizo zilizosimamishwa mwezi Machi baada ya kutinga hatua ya maondoano zitachezwa hadi mshindi apatikane.

Awali, FKF ilikuwa imehofia kwamba huenda zikafutiliwa mbali kutokana na ugonjwa wa corona, lakini kufuatia kupunguka kwa virusi hivyo, kuna matuamini.

“Itabidi mechi za FKF Shield zirejelewe ili tupate timu halisi ya kuwakilisha nchi katika michuano ya Caf, la si hivyo, hatutakuwa na mwaakilishi. Tumeamua lazima mechi zote zichezwe,” alisema Nick Mwendwa ambaye amejitokeza kutetea kiti chake cha Urais kwenye uchaguzi ujao wa kitaifa.

“Tunangojea idhini ya Serikali ili tupange ratiba kulingana na wakati tutakaokuwa nao,” alisema Mwendwa.

“Tumewasilisha mapendekezo yetu lakini hatujajibiwa. Tutakuwa na muelekeo muafaka,” aliongeza.

Kufikia raundi ya 16 bora, AFC Leopards iliibwaga Ushuru kwa 4-2 kupitia kwa mikwaju ya penalti na kusonga mbele baada ya mechi kumalizika kwa sare ya 0-0.

Katika mechi zingine, Ulinzi Stars iliilaza Migori Youth 1-0, huku Kariobangi Sharks wakinyuka FC Talanta ya Supa Ligi kwa 4-1.

Mbali na Kenya Commercial Bank (KCB) waliojiondoa, Gor Mahia walikosa kufika uwanjani kucheza dhidi ya Posta Rangers ugani Afraha, pamoja na Bandari FC ambao hawakufika Mbaraki Stadium kucheza na Sofa Paka.

Bidco United ambao wamepandishwa ngazi pamoja na Nairobi City Stars, walikosa kufika Kianyaga Stadium walikotarajiwa kukutana na Fortune Sacco, pamoja na Keroka Technical University walishindwa kufika uwanjani kucheza na Kisumu All Stars.