Michezo

Mechi za Ligi Kuu ya Wanawake zaahirishwa

February 21st, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

MSIMU mpya wa mwaka 2019/20 wa Ligi Kuu ya Wanawake nchini (KWPL) sasa utaanza Jumamosi Machi 2, 2019 na si Jumapili Februari 24, 2019 jinsi ilivyokuwa imeratibiwa.

Shirikisho la soka nchini (FKF) limetangaza kwamba KWPL imeaihirishwa hadi Jumamosi ijayo huku ikibainika kwamba klabu 16 zinazoshiriki ligi hiyo ziliomba zipewe muda zaidi wa kujifua kwa msimu mpya ili kuhakikisha zinatoa ushindani mkali kwa wapinzani.

Kulingana na ratiba ya msimu mpya, bingwa mtetezi Vihiga Queens wataanza kampeni ya kutetea ubingwa wao dhidi ya Vihiga Leeds katika uwanja wa Mumias Complex.

Washiriki wapya Nyuki Stars na Kibera Girls zitachuana dhidi ya Soccer Queens na Gaspo Youth Mtawalia katika mechi zao za kwanza. Mechi za ligi hiyo pia zitasakatwa siku ya Jumapili.

Nyuki Stars na Kibera Girls i zilijunga na KWPL baada ya kumaliza katika nafasi mbili za kwanza kwenye ligi ya daraja la pili msimu uliopita wa 2018/19.

Hata hivyo mashabiki wanatarajia msimu huu uwe wa kufana baada ya ligi hiyo kusitishwa kwa muda mwezi Septemba mwaka jana kutokana na changamoto za kifedha. Hii ilifuatia hatua ya Shirikisho la soka Duniani(FIFA) linalofadhili KWPL kuchelewa kuwasilisha awamu ya pili ya pesa kwa klabu zote 16 kutumia kuendesha masuala yake.

FIFA hutoa Sh1.2 milioni kwa kila timu inayoshiriki KWPL ili kugharimia oparesheni zake msimu mzima na fedha hizo hutolewa kwa awamu mbili.