Michezo

Mechi za marudiano ya kombe la FA zafutiliwa mbali huku michuano ya nusu-fainali ya Carabao Cup ikiwa sasa ya mkondo mmoja katika msimu wa 2020-21

August 13th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

HAPATAKUWEPO na mechi za marudiano katika Kombe la FA msimu ujao iwapo vikosi vinavyomenyana vitatoshana nguvu na kuambulia sare mwishoni mwa muda wa kawaida.

Aidha, mechi za nusu-fainali za kuwania ubingwa wa Carabao Cup nchini Uingereza sasa zitakuwa za mkondo mmoja pekee muhula ujao.

Maamuzi hayo yanachochewa na haja ya kupunguza mrundiko wa michuano katika ratiba ya soka ya Uingereza msimu ujao.

Mechi za raundi ya kwanza ya mchujo katika Kombe la FA msimu ujao zimepangiwa kuanza mnamo Septemba 1, 2020 huku fainali ikiratibiwa kutandaziwa uwanjani Wembley, Uingereza mnamo Mei 15, 2021.

Michuano wa raundi ya kwanza ya mechi za Carabao Cup itasakatwa kuanzia Septemba 5, 2020 huku mechi za raundi tatu zinazofuata zikipangiwa kupigwa katikati ya wiki kati ya Septemba 15-16, 2020.

Fedha zitakazotolewa kwa washindi wa Kombe la FA katika msimu wa 2020-21 pia zimepunguzwa kwa asilimia 50 kutoka kwa zile ambazo mabingwa wa 2019-20 walipokezwa kutokana na athari za janga la corona.

Washindi wapya sasa watatia kapuni kima cha Sh252 milioni badaya Sh504 milioni zilizotolewa muhula huu.

Droo za mechi za raundi ya kwanza kwenye FA Cup na EFL Carabao Cup zitafanywa mnamo Agosti 18, 2020.

Fainali ya EFL Cup itandaziwa uwanjani Wembley, Uingereza mnamo Februari 28, 2021.

Kampeni za kuwania ubingwa wa EFL Trophy zitaanza Septemba 8-9 kisha fainali kusakatiwa ugani Wembley mnamo Machi 14, 2020.