Michezo

Mechi za nyumbani tukichezea Kisumu tunapata hasara – Gor Mahia

September 18th, 2019 2 min read

NA CECIL ODONGO

MIBABE wa soka nchini Gor Mahia wamefutilia mbali mechi zao zote za nyumbani katika uga wa Moi mjini Kisumu kutokana na kile walichotaja kwamba kupata hasara kubwa kwenye mapato yao.

Mwenyekiti wa K’Ogalo Ambrose Rachier alieleza Taifa Leo kwamba kuna ‘wakora’ ambao wamekuwa wakiendeleza tabia ya kukusanya ada ya kiingilio kwa niaba ya klabu kisha kuzitia mfukoni, tabia ambayo hawataendelea kuvumilia kwa kuwa inawapa hasara kubwa kifedha.

“Kuanzia leo (jana Jumanne), tumesitisha kwa muda mechi zetu zote katika uga wa Moi mjini Kisumu hata kama ndio kitovu cha ufuasi wa timu yetu. Inasikitisha kwamba wakora hawa ambao ni watu wenye miraba minne waliokula wakashiba wamekuwa wakikusanya pesa langoni kisha kuzitia mfukoni na kutupatia hasara kubwa,” akasema Rachier.

Akaongeza: “Kila tunapocheza mechi za nyumbani katika uga huo, mashabiki lukuki huingia uwanjani bila kulipa ada ya kiingilio au mara nyingi hutoa mapeni machache kwa wakora hawa. Ni jambo ambalo hatutaendelea kuvumilia kamwe.”

Hata hivyo, alisema wapo huru kucheza mechi za ugenini katika uga huo kwa kuwa fedha zitakuwa zikikusanywa na timu ya nyumbani wakianza na mechi ya kesho dhidi ya Chemelil Sugar.

Afisa Mkuu Mtendaji wa K’Ogalo Lordvick Aduda aliunga mkono kauli ya Rachier akifutulia mbali dhana kwamba klabu hiyo imekuwa ikikusanya mapato ya juu kila mara inapoandaa mechi ya nyumbani jijini Kisumu.

“Kuanda mechi Kisumu imekuwa hasara kubwa kwetu. Kwa mfano gharama ya mechi ya ufunguzi kati yetu na Tusker FC ilikuwa zaidi ya Sh700,000 ilhali fedha zilizokusanywa ni Sh120,00 pekee. Hili ni jambo lisilokubalika kamwe,” akasema Aduda.

Afisa huyo alisema alilazimika kupiga simu na kuingilia kati mzozo kati ya wakora hao na maajenti wa klabu baada ya lango la kuingia uwanjani kufungwa na watu hao wakitaka walipwe fedha na klabu.

“Walifunga lango na kuwachapa maafisa na maajenti wetu. Tunajua wanapinga mfumo mpya wa kiteknologia wa kulipia mechi lakini sisi hatujali na tutaendelea kutumia mfumo huo. Hawewezi kutuweka mateka ilhali klabu inaendelea kupata hasara nao wakifaidika,” akaongeza Aduda.

Kulingana na Rachier na Aduda mechi zote za nyumbani za K’Ogalo sasa zitasakatwa katika nyuga za Kenyatta, mjini Machakos au MISC Kasarani, Nairobi.