Michezo

Meltah Kabiria mabingwa wa Super 8

November 22nd, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Meltah Kabiria ilitawazwa mabingwa wa Super Eight Premier League (S8PL) baada ya kulipua NYSA mabao 4-0 kwenye mechi ya kusisimua iliyopigiwa BP Stadium, Kawangware, Nairobi.

Melta ya kocha, Urbanus Mwangi ilimaliza kileleni mwa jedwali la kipute hicho kwa kukusanya alama 61, moja mbele ya Githurai Allstars iliyozaba Rongai Allstars mabao 2-1.

Nayo TUK iliinyoa Dagoretti Former Players mabao 2-1 na kukubali yaishe ilipoibuka tatu bora kwa alama 60. Melta iliteremsha mchezo safi mbele ya wapinzani wao na kuzoa ufanisi huo kupitia Collins Omondi aliyepiga ‘Hat trick’ na nahodha wake Wilson Muhoto alipofunga mara moja.

”Hatimaye tulibahatika kubeba ubingwa wa kipute cha muhula huu baada kuupigania ndani miaka minne,” alisema nahodha huyo.

”Natoa mwito kwa wahisani wajitokeze kutupiga jeki kwenye shughuli zetu za kukuza talanta za wachezaji chipukizi mashinani,” mshirikishi wa michezo hiyo, Athanas ‘Obango’ Obala alisema

Melta ndiyo timu ya pili kutoka Kanda ya Nairobi Magharibi kutwaa taji hilo baada ya Kawangware United kulibeba mwaka 2016.

`Nayo Jericho Allstars bingwa wa msimu uliyopita ilimaliza ya sita kwa alama 50 baada ya kutoka sare goli 1-1 na Metro Sports. Mathare Flames ililazimisha sare bao 1-1 mbele ya MASA na kumaliza ya sita kwa alama 53.