Michezo

Meltah Kabiria wamaliza mkondo kwa kishindo

June 25th, 2018 1 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

Meltah Kabiria imemaliza mechi zake za mkondo wa kwanza za Super 8 Premier League kwa kishindo kufuatia ushindi wa 4-2 dhidi ya Shauri Moyo Blue Stars, mwishoni mwa wiki.

Washindi waliokuwa wenyeji kwenye mechi hiyo iliyochezewa Riruta BP Stadium walipata bao la kwanza kupitia kwa Erick Kyalo mapema dakika ya nne.

Sammy ‘Lefty’ Agesa alisawazisha mambo alipomimina wavuni bao dakika ya 14 kutokana na kombora la karibu na eneo la hatari.

Blue Stars waliongeza bao la pili kupitia kwa Idris Gerard, m uda mfupi kabla ya wakati wa mapumziko na kufanya mambo kuwa 2-1 wakati huo wa mapumziko.

Mchezaji nyota Edwin Njire aliifungia Meltah mabao mawili dakika za 54 na  and 85 baada ya kumchanganya kipa Dalton Musa.

Ushindi huo uliwasukuma Meltah hadi nafasi ya tano baada ya kujikusanyia jumla ya pointi 23 kutokana na mechi 15.

“Huu ni ushindi muhumu baada ya majuzi kushindwa na Metro kwa 1-0. Vijana walirekebisha makosa yao na kucheza kwa ushirikiano mkubwa,” alisema kocha wa Meltah, Stanley Njoroge baada ushindi huo wao wa sita.

“Nafurahia jinsi walivyocheza, kila mtu alifanya kazi yake ipasavyo,” aliongeza.

Mechi kati ya Rongai All Stars na Kayole Asubuhi haikuchezwa.

Matokeo ya wikendi kwa ufupi yalikuwa:

Meltah Kabiria 4 Shauri Moyo Blue Stars 2, Shauri Moyo Sportiff 1 Kawangware United 3, Metro Sports 0 RYSA 0, Leads United 1 MASA 0, Zamalek 1 NYSA 2.