Michezo

Mema Foundation Academy inavyonoa vipaji vya soka licha ya changamoto

February 13th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

KLABU ya Mema Foundation Academy ina vijana chipukizi kati ya miaka 9-13 wenye lengo la kukuza vipaji Kaunti ya Kiambu.

Licha ya Klabu hii kukosa ufadhili unaofaa vijana hao wadogo hujibiidisha katika mazoezi katika uwanja wa Kasarini mjini Kiambu ili kunoa makali yao.

Kulingana na kocha wake Tiobath Mugiira, wengi wa vijana hao ni kutoka katika familia maskini, huku lengo lake kuu ni kuwapa maadili mema maishani.

“Vijana wengi wamebadilika mno kutokana na timu hii kudumisha nidhamu na kufuata maagizo ninayowapa,” asema Mugiira.

Kocha huyo anasema timu hiyo iliyobuniwa mwaka wa 2010 inajumuisha wanafunzi wa shule ya msingi ambao wengi wao wametokea kuwa vijana wa kutegemewa katika jamii.

Anasema bali na kuwafunza soka vijana hao wanafunzwa kuelewa miradi tofauti maishani.

“Tuna miradi kama ya ufugaji wa samaki, upanzi wa miti, na hata ufugaji wa ng’ombe ili kuelewa jinsi ya kukamua maziwa,” anasema Mugiira.

Lengo kuu hasa ni kuwaepusha vijana hao kujitumbukiza katika anasa na utumizi wa mihadarati ili kuwafanya kuwa raia wema katika siku za usoni. Picha/ Lawrence Ongaro

Kwa wakati huu vijana hao wanashiriki katika mashindano ya Rising Stars Junior League, inayoendelea katika viwanja vya HillCrest School, na Utalii College jijini Nairobi.

Kulingana na kocha Mugiira, mashindano hayo yataendelea kwa muda wa msimu wote wa 2019 hadi mwezi Desemba wakati watampata mshindi kamili wa Ligi hiyo.

Alisema shule za kibinafsi zipatazo 60 zimejitokeza kushiriki huku vijana wa malezi Mema Foundation Academy wakiwa wa pekee wa kujitegemea .

“Mimi kama kocha wa vijana wangu nilionelea kuwaingiza Ligini ili watangamane vyema na vijana wenzao kutoka shule za kifahari,” alieleza.

Mashindano hayo yamedhaminiwa na shirika la Soccer Academy Accenture kutoka  Nairobi.

“Hata hivyo anasema mikakati ya kukwea mlima wa soka ya humu nchini hudidimizwa na ukosefu wa ufadhili wa kugharimia mahitaji muhimu,”Mimi kama kocha nimekuwa nikitumia fedha zangu za mfukoni kuwaleta pamoja watoto wasiojiweza kimaisha,” asema.

Anatoa mwito kwa wafadhili wanaoweza kujitokeza wafanye hivyo ili aweze kuwasaidia vijana hao kupiga hatua zaidi.

“Licha ya kukabwa na mahitaji mengi ya kibinafsi bado ninafanya juhudi kuona ya kwamba ninashughulika na vijana hao,” alisema Bw Mugiira.