Makala

'Meme Lord' asimulia alivyojinasia penzi mitandaoni

April 30th, 2020 2 min read

NA STEVE MOKAYA

Shem Obare, almaarufu ‘Fantacy the Meme Lord’, ni mwanafunzi wa mwaka wa nne katika Chuo Kikuu cha Dedan Kimathi, Nyeri anayesomea taaluma ya uuguzi.

Fantacy alianza kutengeneza memes baada ya kuachana na mpenziwe; baada ya kumaliza kidato cha nne, mwaka wa 2015.

Jambo lililoanza kama mzaha wa kujisahaulisha tabu za mapenzi chaju limekua kwa kasi na sasa hivi ‘Fantacy’ anajulikana na watu wengi mtandaoni. Alizungumza na Dijitali Taifa Leo, na kuelezea pandashuka za kuunda memes.

“Mwanzoni nikianza, nilikuwa natumia jina ‘The Real Memelord’. Hapo nilikuwa na wafuasi wachache tu. Halafu, wakati mmoja nikatengeneza meme fulani ambayo ilisambazwa kwenye mitandao sana. Ilinipa mshawasha zaidi hadi nikaamua kujipa jina la jipya la ‘kikazi’, ‘Fantacy the Meme Lord,”’ anaeleza.

Kadri alipozidi kujulikana kupitia kwa kazi zake, ndipo ufuasi wake katika kurasa za mitandao ya kijamii ulipokua.

“Nilipofungua ukurasa wa memes kwenye Facebook, nilikuwa na ‘likes’ themanini. Ila saa hii zimeongezeka hadi laki moja na elfu kumi. Kadhalika, kwenye Instagram niko na ufuasi wa zaidi ya watu elfu arubaini na sita,” anaeleza.

Ufuasi huu mkubwa ulianza kuvutia wafanyabiashara na kampuni mbalimbali ambazo zinamtaka awafanyie matangazo ya biashara zao katika kurasa zake, kwa malipo.

“Miezi michache iliyopita kulikuwa na uhaba wa nyanya humu nchini, na kufanya bei yake kupanda kwa kiasi kikubwa. Wakati huo, kampuni moja ya kutengeneza tomato paste ilinipa kazi ya kuwatengenezea memes za kuwatangazia bidhaa yao, na wakanipa fedha zilizonisukuma huko chuoni,” anaeleza.

Mbali na kupata faida za hela, kujulikana sana, pia kazi hii ilimsaidia kupata mpenzi. Anaeleza ilivyokuwa.

“Tuko na vikundi vya Whatsapp na Facebook vya wacheshi wa vikatuni. Wakati mmoja, binti mmoja akanitumia ujumbe na tukaanza kuongea. Mwanzo alikuwa anahitaji msaada wa ushauri wa jinsi ya kuboresha memes zake ziwe kama zangu. Baada ya siku kadhaa za kuongea, mapenzi yakaanza kuota. Hivi sasa yeye ndiye mpenzi wangu,” anasema akicheka.

Halikadhalika, wanafunzi wenzake chuoni anakosoma, hasa wale wanaowania vyeo mbalimbali vya uongozi wa wanafunzi huwania huduma zake wakati wa kampeni.

“Ninawatengenezea memes za kuwafanyia kampeni, na wao hunipa kitu kidogo,” anasema.

Kadhalika, kutokana na kazi hii, Shem Obare amejulikana sana chuoni mwao na hilo pekee humpa raha.

Hata hivyo, anakiri kuwa kazi ya kutengeneza memes huhitaji ufahamu wa mambo yanayojiri kwa wakati fulani. Anasema kuwa ili memes ziweze kusambazwa kwa wingi na kupendawa na wengi, ni lazima ziwe za maana na ziende sambamba na yale yanayojiri katika jamii. Yeye anasema kuwa hupata yanayojiri kwa wakati kupitia kwa mtandao wa Twitter.

Hata hivyo, Fantancy anakiri kuwa zipo changamoto katika kazi hii.

“Wakati mwingine ninakosa mahali pa kutoa michezo, yaani content. Halafu pia wakati mwingine unapata kuwa memelords wengine huiba kazi zako na kuzifanya kuwa kama zao. Unakufa moyo wakati mwingine, ila unabidi uzoee,” anasema.

Isitoshe, ujumbe unaoweka katika memes unaweza kuwa unaudhi watu fulani, jamii kwa jumla au hata serikali. Anaeleza kisa kimoja cha aina hiyo.

“Kuna wakati video ya ngono ilikuwa imetolewa kwa umma kupitia kwa mitandao ya kijamii. Sasa mimi nikaitumia kutengeneza meme. Kishaye nikaeweka kwenye Facebook. Haikukaa kwa muda kabla ya kutolewa na usimamizi wa Facebook. Kwa hivyo, ni lazima uwe makini usije ukatengeneza memes ambazo zinakosa maadili, au zinazoweza kusababishia hata kesi mahakamani,” anasema.

Fantacy anasema kuwa, ili kuimarisha memes zake, anatengeneza zile ambazo zinahitaji mtu kufikiria zaidi ili apate kuona ucheshi uliomo. Kadhalika, ako na mipango ya kuanza kutengeneza video za ucheshi.

“Tayari nimepata watu wanaotaka niwafanyie kazi hiyo,” anasema.