Michezo

Menaja wa Butterfly FC awataka marefa kukomesha mapendeleo

March 11th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

MENEJA wa Butterfly FC Fredrick Ndinya ametoa mwito kwa waamuzi wa mechi za soka nchini kutekeleza wajibu wao bila mapendeleo ili kuimarisha kiwango cha mchezo huo.

Afisa huyu alidokeza haya muda mfupi baada ya timu hiyo kupondwa mabao 3-2 na Gor Mahia Youth kwenye mechi ya Kundi C Ligi ya Taifa Daraja ya Pili iliyochezewa uwanjani City Stadium, Nairobi.

”Mfungaji wa bao la pili Gor Mahia Youth, Llyod Kavuchi alikuwa ameotea lakini ilionekana mwamuzi wa katikati alifumba macho kuacha mechi iendelee,” meneja huyo alisema na kuongeza kwamba Gor Mahia Youth nyakati nyingi husaidiwa kushinda wapinzani wao.

Gor Mahia Youth ilitwaa ufanisi huo kupitia juhudi zake Llyod Kavuchi aliyegaragaza mbili safi naye Oyugi Alfayo aliifungia bao moja huku Teddy Otieno na Paul Wamalwa wa Butterfly kila mmoja akitikisa nyavu mara moja.

Butterfly ilidondosha pointi mbili muhimu baada ya kunyanyua Gogo Boys mabao 2-1 wiki iliyopita. Nao limbukeni wa Gor Mahia Youth walikuwa wamedhalilisha Kibra United kwa magoli 5-0.

Nao wachezaji Reuben Onsando, Geooffrey Adero na Kennedy Mutesa kila mmoja alifanikiwa kuchekana na nyavu mara moja na kubeba Tandaza FC kuchoma Gathanga FC mabao 3-0. Kwenye mchezo mwingine, Kibera United iliiponda Mathaithi mabao 2-0 kupitia Billy Nyaoro huku Gogo Boys ikitoka sare tasa na CMS Allstars.