Michezo

Mendy kuchezea Leicester City hadi 2022

August 25th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIUNGO Nampalys Mendy wa Leicester City amerefusha muda wa kuhudumu kwake uwanjani King Power kwa miaka miwili zaidi.

Sogora huyo mwenye umri wa miaka 28 alijiunga na Leicester mnamo 2016 baada ya kukatiza uhusiano wake na Nice ya Ufaransa.

Alihudumu ugani King Power kwa mwaka mmoja kabla ya kurejea Nice kwa mkopo wa msimu mmoja mnamo 2017-18.

Mkataba wa awali kati ya Mendy na Leicester ulitarajiwa kutamatika Juni 2020.

Hata hivyo, kikosi hicho kilichokamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika nafasi ya tano, kilirefusha kandarasi yake hadi mwishoni mwa msimu huu uliorefusha kwa sababu ya janga la corona.

“Nimeridhishwa na uwezo wake uwanjani na benchi ya kiufundi imeamua kuendelea kujivunia huduma zake kwa miaka miwili zaidi,” akatanguliza kocha Brendan Rodgers.

“Kuwa na mchezaji kufu ya Mendy kambini ni nafuu tele. Ana tajriba pevu na ukomavu wake katika safu ya kati ni mhimili mkubwa na kiini cha hamasa ambayo kwa sasa inawavaa chipukizi wote kambini,” akaongeza kocha huyo wa zamani wa Liverpool na Celtic.

Mendy amechezea Leicester jumla ya mechi 29 hadi kufikia sasa msimu huu wa 2019-20.