Makala

MENDYLENE WAIGWEHIA: Nawashangaa maprodusa wasioipenda Kenya

January 24th, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

INGAWA tangia akiwa mtoto alitamani kuhitimu kuwa mhudumu katika ndege, sasa anapania kuibuka kati ya wasanii mahiri Afrika kama Jackie Appiah ambaye hushiriki filamu za Kinigeria (Nollywood).

Msanii huyo ambaye ni mzawa wa Canada ni miongoni mwa waigizaji waliobobea nchini Ghana.

Mendylene Wanjiku Waigwehia ambaye kisanaa anafahamika kama Shikoo anasema alivutiwa na uigizaji akiwa mdogo lakini alipata motisha zaidi baada ya kutazama kipindi cha Mother-in law ambacho hupeperushwa kupitia Citizen TV.

Ingawa hajapata mashiko katika masuala ya maigizo anasema anatamani zaidi kuibuka kati ya wasanii mahiri nchini miaka ijayo. Kando na sanaa ya maigizo kipusa huyu amezamia zaidi katika taaluma ya msanii mpodoaji pia ni msusi.

”Sio siri mimi nimefanya kazi nyingi kama mpodoaji ambapo huwapodoa wana harusi bila kusahau wateja wa kawaida,” anasema mwana dada huyo na kuongeza kuwa ni miongoni mwa ajira zinaweza kusaidia wahusika kujikimu kimaisha.

Anasema alianza kujituma kwenye masuala ya maigizo mwaka 2010 ambayo huzalisha filamu wakitumia mwongozo wa vitabu vya riwaya. Msichana huyu amefanya kazi na makundi kama Theatrolix Quality Production na Zuia Theaters and Cultural Organization kati ya mengine.

Anawaponda maprodusa wa humu nchini maana hawapendi kuzalisha filamu zinazohusu utamaduni wetu ili kuvutia watazamaji wa nyumbani.

”Kwa mtazamo wa wengi wetu suala la kupuuza utamaduni wetu ndilo nimefanya wananchi wengi kuvutiwa na filamu za kigeni,” alisema na kuongeza kuwa hatua hiyo huwa inabomoa kazi za waigizaji wazalendo.

Demu huyu anasema hapa nchini angependa kufanya kazi na wasanii kama:Victoria Muthigi, Brenda Wairimu na Annette Odusi kati ya wengine.

Kwa waigizaji wa Nollywood anadai kando na Jackie Appiah pia angependa sana kushirikiana na Ini Edo ambaye ameshiriki zaidi ya filamu 100 tangu mwaka 2000 alipojiunga na uigizaji. Edo anajivunia kuteuliwa kuwa jaji mwaka 2013 kwenye mashindano ya urembo ya miss Black Afrika UK Pageant.

”Bila kupaka mafuta kwenye mgongo wa chupa waigizaji wa kike nchini hupitia mazito ambayo huwavunja moyo wengi na kuyeyusha matamanio yao,” anasema na kuongeza kwamba katu hawapaswi kusepa haraka bali wanastahili kujituma bila kulegeza kamba.

Binti huyu anaziomba serikali za Kaunti kote nchini kuwazia mpango mwafaka kusaidia sekta ya filamu hapa Kenya. Anachana waigizaji waliotangulia na kusisitiza kwamba ubinfasi umetawala miongoni mwao na kuzima ndoto za wasanii wanaoibukia.

Dada huyu siyo mchoyo wa mawaidha. Anahimiza wenzake kwamba wanastahili kujiepusha na mahusiano ya kimapenzi dhidi ya waigizaji wenzao maana suala hilo huwashusha hadhi wanawake.

Anadokeza kwamba mahusiano sapuli hiyo hatimaye huambulia patupu maana wanaume husepa huku wanawake wakiachwa kwa mataa.