Habari Mseto

Meneja akana kupanga njama ya kutafuna mamilioni ya Naivas

November 11th, 2020 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MENEJA wa Fedha alishtakiwa kwa kukula njama za kuifilisi duka la supa la Naivas zaidi ya Sh33.8 milioni.

Dennis Muchina Thiaka, alikana mbele ya hakimu mkazi Bi Jane Kamau kwamba akishirikiana na watu wengine ambao hawakuwa kortini  kulaghai duka la jumla la Naivas Sh33,808,985 kati ya 2016 na 2020.

Thiaka mwenye umri wa miaka 32 aliomba korti imwachilie kwa dhamana akisema yuko na mke na watoto wanaomtegemea yeye.

Alieleza korti atafika kortini siku ya kusikizwa kwa kesi inayomkabili.

Upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili wa serikali Fredrick Kimathi hakupinga ombi la mshtakiwa ila aliomba korti itilie maanani kiwango cha pesa ambacho kingelipotea.

Akimwachilia hakimu alisema dhamana ni haki ya kila mshukiwa. Alisema upande wa mashtaka haupingi akiachiliwa kwa dhamana na kumwagiza alipe dhamana ya pesa tasilimu ya Sh500,000.

Pia alimwagiza jamaa wake afike kortini kutia sahini cheti kwamba atahakikisha mshtakiwa amefika kortini siku ya kusikizwa kwa kesi.

Kesi itatajwa tena Novemba 24. Bw Thiaka ameajiriwa na kampuni ya Achievo inayotoa huduma za uhasibu kwa maduka haya ya Naivas.