Bambika

Meneja alia kukaushwa tangu Stevo Simple Boy azirai kwenye runinga

April 5th, 2024 2 min read

NA FRIDAH OKACHI

CHINGIBOY Mstado ambaye ni meneja wa msanii Stephen Otieno Adera almaarufu Stivo Simple Boy amefichua kutokuwa na maelewano mazuri na msanii huyo, kizingiti kikiwa ni familia ya msanii huyo, tangu tukio la kuzirai akiwa anatumbuiza jukwaani kwenye runinga moja nchini.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo Dijitali, Chingiboy alifichua kuwa tangu tukio hilo, hajawahi kukutana ana kwa ana na msanii huyo wala kuzungumza naye kupitia njia ya simu.

Alilalamikia familia ya msanii huyo, kukatiza mazungumzo baina yake na msanii huyo.

“Ni wiki mbili sasa, Stivo Simple Boy alipoanguka akitumbuiza mashabiki wake. Wakati wa tukio hilo familia yake ilikuja na kumchukua na kuenda naye hadi leo sijapata fursa ya kuongea naye,” alinug’unika meneja huyo.

Chingiboy alisema amekuwa akipitia mahangaiko kutoka kwa familia ya msanii huyo.

“Simu yake imefungwa na unapompigia haipokelewi,” alisema.

Meneja huyo aliyeanza kufanya kazi naye Mei, 2023, alishangazwa na jinsi familia yake ilimtuhumu kwa kula jasho la msanii huyo akisema yeye hutumia hela zake binafsi kufanikisha mishemishe za Simple Boy.

“Familia yake inaona nafyonza jasho la msanii huyu. Mimi binafsi nilitumia hela zangu ili kuhakikisha hadhi yake haishuki. Ndiposa nimemkutanisha na wanasiasa kumpadisha. Kabla kupakulia mashabiki ngoma mwezi jana, nilimpeleka kwa Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino kwa gharama yangu kuhakikisha ngoma tuliyozindua itashabikiwa na wengi,” alijitetea Chingiboy.

“Familia yake iliona kukutana na Babu Owino tulipewa pesa lakini sivyo. Nilitaka Kiki tuu,” alifafanua meneja huyo.

Meneja huyo alilalamikia familia ya msanii huyo kumhamisha mtaa wa Buruburu na kumrejesha katika mtaa wa Kibra.

“Mwezi jana, walikuwa wamemwambia achukue vitu vyote vya nyumba awapelekee. Inaniumiza kuona msaada wangu sio wa maana kwake.

“Stivo ni rafiki yangu na alipoachwa na meneja wa kwanza, aliniomba kufanya kazi naye. Niliona itakuwa vyema kumfikia mheshimiwa Peter Salasya ambaye alimlipia nyumba kwa miezi mitatu na kununua kila kitu kwa nyumba,” alisema Chingiboy.

Taifa Leo ilimtafuta Bw Fred Odero ambaye ni kakaye msanii huyo. Bw Odero alithibitisha tayari msanii huyo ako nyumbani kwake na kususia kutaja mtaa alipo.

“Stivo niko na yeye. Nataka atulie na kisha atafakari. Kwa sasa hataonekana machoni mwa umma hadi awe sawa,” alisema Bw Odero.

“Sitasema anapoishi kwa sasa. Huyo anayesema amerudi Kibra apige picha. Hii nchi ina sheria na ni vyema sheria ifuatwe. Iwapo anahisi chake kimechukuliwa aende mahakamani,” alikamilisha Bw Odero.