Dondoo

Meneja apoteza kazi kwa kutafuna vipusa kazini

Na JANET KAVUNGA June 28th, 2024 1 min read

BAMBURI, MOMBASA

KALAMENI mmoja alipoteza kazi ya meneja wa hoteli baada ya wafanyakazi vipusa kulalamika kwa mwajiri wao kwamba alikuwa akiwasumbua akitaka wamlishe uroda.

Jamaa alikuwa akirushia vipusa mistari na kuanza kuwahangaisha wakikosa kumeza chambo.

SOMA PIA: Mdogo kazini afutwa kazi akibishania mwanamke na mkubwa wake

Kitumbua chake kiliingia mchanga juzi, vipusa aliokuwa akinyanyasa na aliopendelea walipomweleza mwenye hoteli aliyemtimua kwa kupotoka kimaadili.

Wakati huo huo, huko Mtwapa, Kilifi, mwandada alimkemea rafiki yake akimlaumu kwa kumshawishi kaka yake asimuoe.

Urafiki wa wawili hao ulianza wakiwa wanafunzi wa sekondari na demu hakutarajia mwenzake angemchomea picha kwa kaka yake alipokubali kuwa mpenzi wake.

SOMA PIA: Demu ajiondoa kwa chamaa cha vidosho wanyemeleaji wa mabwana

“Demu alipata habari kwamba mwenzake alimuonya kaka yake dhidi ya kumuoa. Alimpaka tope akisema anapenda pesa sana na angemuacha iwapo angefilisika.

Alipopata habari hizo, mwanadada alimkabili wifiye mtarajiwa na kumchemkia kwa hasira kwa kumharibia uhusiano wake na kaka yake,” alisema mdokezi.

Wawili hao walirushiana cheche kabla ya mashoga wao kuingilia kati na kuwatuliza.