Habari Mseto

Meneja wa duka ashtakiwa kuiba bidhaa za mifugo za thamani ya Sh67m

February 18th, 2024 1 min read

NA RICHARD MUNGUTI

MENEJA mmoja wa duka alishtakiwa Ijumaa kwa wizi wa bidhaa za kutibu mifugo za thamani ya Sh67 milioni.

Mali hiyo iliyoibwa inahusishwa na waziri katika serikali ya Kenya Kwanza.

Bw Hussein Ismail Godad kutoka Kaunti ya Garissa alishtakiwa kwa kuiba bidhaa mbalimbali kutoka kwa kampuni ya Medina.

Godad alishtakiwa mbele ya hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Bernard Ochoi.

Bw Ochoi alifahamishwa na kiongozi wa mashtaka James Gachoka kwamba Godad alikuwa meneja wa stoo za kampuni ya Medina Chemicals Limited iliyoko jijini Nairobi alipotekeleza uhalifu huo.

Bw Gachoka alieleza korti Godad aliiba bidhaa mbalimbali za tiba za mifugo mnamo Januari 17, 2024.

Thamani ya bidhaa anazodaiwa kuiba Godad ni Sh67,513,761 mali ya Medina Chemicals Limited.

“Mshtakiwa alizifikia bidhaa hizo kutokana na kazi yake katika kampuni hiyo,” Bw Gachoka alimweleza hakimu.

Bw Godad aliomba aachiliwe kwa dhamana akisema “nimeoa na nimejaliwa watoto ambao ninawakimu kimaisha.”

Mshtakiwa aliahidi kutii maagizo atakayopewa na mahakama ya dhamana.

“Nitatii masharti nitakayopewa na hii mahakama ikiniachilia kwa dhamana,” Bw Godad alieleza korti kwa unyenyekevu mwingi.

Bw Gachoka hakupinga ombi hilo ila alieleza mahakama itilie maanani thamani ya bidhaa zinazodaiwa kuibwa.

Akitoa uamuzi, Bw Ochoi alisema amezingatia kwamba upande wa mashtaka haupingi mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana.

Pia hakimu alisema dhamana ni haki ya kikatiba ya mshtakiwa.

Bw Ochoi alisema mahakama inaweza tu kutwaa haki ya mshukiwa ya kuachiliwa kwa dhamana endapo atatoroka ama ni hatari kwa usalama kwa mashahidi.

Alimwachilia kwa dhamana ya Sh10 milioni na mdhamini mmoja wa kiasi sawa na hicho.

Bw Ochoi pia alimpa mshtakiwa dhamana ya pesa taslimu Sh5 milioni endapo hatapata dhamana ya Sh10 milioni.

Pia hakimu aliamuru upande wa mashtaka umkabidhi mshtakiwa nakala za mashahidi ajue jinsi atakavyojitetea.

Bw Ochoi aliamuru kesi hiyo itajwe Februari 28, 2024, kutengewa siku ya kusikilizwa.