Habari Mseto

Meneja wa mwigizaji Wendy kubakia seli

September 3rd, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MKUFUNZI wa mwigizaji maarufu, Wendy Waeni alizuiliwa jana kwa siku tano kuhojiwa kwa madai alighushi barua aliyodai imeandikwa na Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i.

Bw Joseph Mwangi Nduta almaarufu Joe, aliamriwa azuiliwe katika kituo cha polisi cha Muthaiga kujibu maswali ya kutoa vitisho kwa Waeni na mama yake Magdalene Syombua.

Akiamuru Mwangi azuiliwe, hakimu mwandamizi Bw Bernard Ochoi, alisema mshukiwa huyo alitiwa nguvuni Jumatatu baada ya kujificha kwa wiki kadhaa huku akisakwa na polisi.

Kiongozi wa mashtaka Everlyn Maika. Picha/ Richard Munguti

Bw Ochoi alisema kiongozi wa mashtaka, Bi Everlyn Maika amewasilisha ushahidi wa kutosha kwamba mshtakiwa anajaribu kutoroka kwa sababu anajua makosa aliyofanya ni mabaya.

“Upande wa mashtaka umethibitisha kwamba Mwangi amekuwa akiwakwepa polisi tangu alipopata fununu anasakwa kwa kumnyanyasa Wendy na kutoa vitisho kwa mama yake,” alisema hakimu akitoa uamuzi.

Hakimu mwandamizi Bernard Ochoi. Picha/ Richard Munguti

Bw Ochoi alipuuzilia mbali ushahidi wa Mwangi kwamba hakuwa mafichoni ila alikuwa anahofia maisha yake.

Akiomba mshukiwa huyo azuiliwe kwa siku saba, Bi Maika alimweleza hakimu kuwa Mwangi alizima simu zake zote na kujificha baada ya habari kuchipuka kuwa alikuwa anasakwa. Bi Maika alisema polisi walipokea habari kuwa mshukiwa huyo alikuwa anataka kutorokea Uingereza.