Habari Mseto

Meneja wa zamani apatwa na hatia ya kutafuna Sh62.7 milioni

September 15th, 2020 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA meneja wa kampuni bima amepatikana na hatia ya wizi wa Sh62.7milioni miaka 15 iliyopita.

Hakimu mkuu mahakama ya Milimani Bw Francis Andayi alimpata Lincolin Kivutu Njeru aliye na umri wa miaka 58 na hatia ya wizi wa Sh62,704 , 835.60 kutoka kwa akaunti za mwajiri wake Insurance Company East Africa (ICEA).

Bw Andayi alisema kuwa mshtakiwa alikuwa anapokea pesa kutoka kwa akaunti za ICEA akidai ni kuwekeza katika kampuni ya hisa iliyofilisika ya Nyaga Stock Brokers (NSB).

Hakimu alisema upande wa mashtaka ukiongozwa na Angela Fuchaka ulithibitisha kuwa Njeru aliiba mamilioni ya pesa.

“Njeru hangeweza kueleza jinsi alivyojipatia mamilioni ya pesa alizokutwa nazo katika akaunti zake,” alisema Bw Andayi katika uamuzi aliosoma kwa muda wa nusu saa.

Mahakama ilisema ripoti ya uhasibu iliyonyesha jinsi pesa zilivyoibwa kutoka kwa akaunti ya za ICEA katika benki ya HFCK na kupelekwa Benki ya Barclays na hatimaye katika akaunti za NSB ambapo mshtakiwa aliziiba.

Mahakama ilisema mshtakiwa alidai ni uwekezaji mbaya uliofanya pesa hizo za ICEA kutoweka lakini “ mahakama ikasema pesa zilizowekwa katika akaunti za NSB zilionekana lakini mamilioni mengine ambayo wahasibu walihoji zilipatikana katika akaunti za mshtakiwa.”

Akijitetea kupitia kwa wakili Stanley Kang’ahi, mshtakiwa alisema ameoa kwa kwa muda wa miaka 12 hajakuwa na kazi rasmi.

Mshtakiwa aliomba aadhibiwe kwa kuangizwa atumikie kifungo cha nje.

Hakimu aliamuru idara ya urekebishaji tabia imhoji mshtakiwa kubaini hali yake.

Kiongozi wa Mashtaka Angela Fuchaka aliomba korti “ichukulie hilo kuwa kosa la kwanza la kiuhalifu mshtakiwa kutenda.”

Bw Andayi alifutilia mbali dhamana ya mshtakiwa na kuamuru awekwe ndani

Mahakama iliamuru mshtakiwa azuiliwe katika kituo cha polisi cha Capital Hill hadi Ijumaa atakaporudishwa kortini kuhukumiwa.