Michezo

Menengai Oilers mabingwa wa Great Rift Top Fry 10 Aside

April 29th, 2019 2 min read

NA RICHARD MAOSI

Kikosi cha Menengai Oilers wachezaji kumi kila upande, walinyakua ubingwa wa Great Rift Top Fry 10 Aside wikendi katika uwanja wa Nakuru Athletics Clubs.

Oilers walinyanyua taji baada ya kukalifisha mahasimu zao wa siku nyingi Menengai Top Cream Homeboyz, katika ngarambe ya kukata na shoka.

Homeboyz walikuwa wa kwanza kufunga,kabla ya mapumziko lakini Menengai Oilers walirejea kwa kishindo na kusawazisha kabla ya kupata pointi za ushindi 10-5.

Mbali na kukabiliana na ushindani mkali katika mchujo,dhidi ya KCB,Blak Blad,na Nondes ,Menegai walijizatiti na kuweka hai matumaini yao kufika fainali.

Mashabiki wa Menengai Oilers wakishangilia timu yao ya nyumbani. Picha/Richard Maosi

Michuano hiyo iliyochukua siki tatu kukamilika ilishuhudia ushindani mkali huku timu zikijumuishwa katika makundi matano ya kushindana.

Mashabiki kutoka kila sehemu ya nchi walimiminika kushabikia timu zao,na kujaza nyuga zote,muda wa siku zote,ili kuwapatia mori wachezaji.

Wenyeji Top Fry Nakuru RFC,Kiambu RFC,Moi University,Stingers na Technical University of Kenya(TUK) ,zilikuwa ni baadhi ya timu zilizoibua msisimko wa aina yake,wakiwa limbukeni waliokuja mchezoni kwa mara ya kwanza.

Timu hizi zilipanda daraja,kutoka ligi ya chini baada ya kuwaondoa vigogo,katika awamu za mchujo zinazoandaliwa na Kenya Rugby Union(KRU).

Chrispine Shitundo wa Menengai Oilers akiwazidi maarifa wachezaji wa Mean Machine uwanjani Nakuru Athletics Club. Picha/ Richard Maosi

Nakuru RFC waliratibiwa kuumiza nyasi katika kundi A ,pamoja na Meru RFC,KPA Eldoret na Chuo Cha Bomet.

Katika kundi B,Chuo kikuu cha Moi waliorodheshwa na Nothern Suburbs ,Dagoretti Bull Dogs pamoja na Kenya School of Law.

Kwenye kundi C kiambu RFC wakatifua kivumbi dhidi ya Muranga RFC,Molo na Vihiga Granites.

Kundi D Stingers walimaliza kazi waliporatibiwa kushindana na,Chuo Cha KCA,Zetech na Brumbies RFC.

Wachezaji wa KCB wakiwania mpira dhidi ya Egerton Wasps. Picha/ Richard Maosi

Hatimaye kundi E ilikutanisha vigogo Technical University,Administaration Police ,Nakuru KITI na Citam kutoka kaunti ya Kisumu.

Chuo Kikuu cha Masinde Muliro MMUST walichukua nambari tano,katika mashindano yote baada ya kunyamazisha Strathmore Leos 35-10,katika pambano la awali.

Blak Blad,wanafunzi kutoka Chuo cha Kenyatta nao hawakubaki nyuma,waliposhangaza KCB 7-5,huku Homeboyz wakitandika Stingers 5-0.

Kwenye mechi ya fainali iliyokutanisha Menengai Oilers na Homeboyz,Menengai walitamba huku wakiangushia Homeboyz kwa kichapo kikali cha 10-5.

Homeboyz ambao ni mabingwa watetezi walishindwa kuhifadhi taji lao,waliloshinda msimu uliopita wakiridhika na nafasi ya pili.

Hata hivyo mkufunzi wao Simon Odongo,alikubali matokeo akisema timu ieweka mikakati kuboresha matokeo siku za usoni.

Duncun Abuyeka (kushoto) akingangania mpira dhidi ya mchezaji wa Mean Machine uwanjani Nakuru Athletics Club. Picha/ Richard Maosi

Mkufunzi wa Homeboyz Simon Odongo aliwamiminia sifa vijana wa Menengai Oilers kwa kupindua matokeo ya awamu ya 28 yaliyofanyika mnamo 2018.

Kwingineko katika ligi ya divisheni ya pili,Nakuru RFC walinyanyua taji baada ya kukalifisha Stingers 5-0.

Nao wanafunzi kutoka Chuo Kikuu Cha Eldoret(UOE),waliambulia nambari 13 baada ya kuandikisha msururu wa matokeo mazuri katika ligi ya divisheni ya pili.

Kufikia sasa UOE wamejihakikishia nafasi ya kushiriki michuano ya Kenya Cup kuanzia mwaka ujao.

Katika orodha ya wachezaji bora msimu huu,Brian Songoi wa Homeboyz aliibuka kuwa mchezaji kidedea wa raga wachezaji 10 kila upande.

Derrick Mbaire wa Menengai Oilers akiibuka kuwa mchezaji wa thamani kubwa katika jumuia ya mashindno ya wachezaji 10 kila upande 2018/2019.

Miongoni mwa wachezaji wengine waliotamba ni pamoja na Charles Omondi(Top Fry),Samwel Mbeche wa Masinde Muliro,Duncun Abuyeka na Hannington Wabwire wa Top Fry.