Habari Mseto

Mercy Cherono afanyiwa upasuaji wa mguu

June 13th, 2020 1 min read

NA ERIC MATARA

Mercy Cherono, mwanamke aliyedhulumiwa na polisi eneo la Olenguruone kaunti ya Nakuru alifanyiwa upasuaji wa mguu jana katika hospitali kuu ya Nakuru.

Muuguzi mmoja aliambia Taifa Leo kwamba Bi Cherono alifanyiwa upasuaji katika mfupa uliokuwa umevunjika. Wauguzi walisema kwamba walikuwa na mikakati thabiti ili kuzuia idadi ya watu wanaomtembelea.

“Alifanyiwa upasuaji na wanaoruhusiwa kumtembelea ni wachache. Amepewa wakati ili apumzike na kupona,” muuguzi alisema.

Bi Cherono alihamishwa kutoka hospitali ya Olenguruone hadi hospitali ya Nakuru Alhamisi.

Wawakilishi wa chama cha wanawake FIDA na viogozi wachache ndio waliruhusiwa kuingia.

Mkurungezi wa Fida Anne Ireri, aliyeongea baada ya kumtembelea jana alikemea jambo hilo na kuwaomba serikali iharakishe uchunguzi ili mwathiriwa apate haki.

“Tumeteua wakili atakayefuatilia na kuhakikisha Mercy amepata haki. Waliohusika lazima wahukumiwe kisheria kama watapatikana na hatia,” alisema.

Bi Ireri alisema kwamba Fida itampa ushauri, nasaha na tiba. Katika Hospitali ya Nakuru Afisa wa polisi ameteuliwa ili kulinda wadi hiyo.