Michezo

Messi acheka na nyavu katika ushindi mwembamba wa Barcelona dhidi ya Levante

December 14th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

LIONEL Messi alifungia Barcelona bao la pekee na la ushindi dhidi ya Levante katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mnamo Jumapili.

Martin Braithwaite, Clement Lenglet, Jordi Alba na Antoine Griezmann walipoteza nafasi kadhaa za kucheka na nyavu za Levante waliomtegemea pakubwa kipa Aitor Fernandez kupangua makombora ya masogora hao wa Barcelona.

Bao lililofungwa na Messi lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na kiungo mkabaji, Frenkie de Jong.

Jaribio la pekee la Levante langoni mwa Barcelona lilikuwa kombora lililovurumishwa na Jorge de Frutos ambaye alishirikiana na Son kabla ya kumtatiza kipa Marc-Andre ter Stegen katika kipindi cha pili.

Ushindi huo uliokuwa wa tano kwa Barcelona kusajili hadi kufikia sasa msimu huu, uliwakweza hadi nafasi ya nane kwenye msimamo wa jedwali la La Liga.

Ni matarajio ya kocha Ronald Koeman kwamba matokeo hayo yatachochea zaidi wanasoka wake kuwaangusha viongozi Real Sociedad watakaokutana nao mnamo Disemba 16 uwanjani Camp Nou.

Barcelona walishuka dimbani wakitawaliwa na kiu ya kusajili ushindi baada ya kushuhudia rekodi mbovu iliyowashuhudia wakipepetwa 1-0 na Cadiz katika mechi ya awali ligini kabla ya Juventus kuwapokeza kichapo cha 3-0 katika mchuano wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Disemba 8, 2020.

Bao la Messi lilikuwa lake la nane hadi kufikia sasa kwenye kampeni za La Liga muhula huu. Levante walisalia katika nafasi ya 18 jedwalini kwa alama 11 sawa na Huesca na Osasuna wanaovuta mkia.